RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kikazi ya siku moja nchini Comoro kesho Jumapili tarehe 6 Julai, 2025 kwa mwaliko wa Rais wa Umoja wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Azali Assoumani.
Rais Dkt. Samia atahudhuria Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa nchi hiyo zitakazofanyika katika Uwanja wa Malouzini Omnisport mjini Moroni, ambako anatarajia kuhutubia kwenye sherehe hizo.
Tangu nchi hiyo ipate Uhuru mwaka 1975, Tanzania na Comoro zimeendelea kudumisha uhusiano wa kidugu na wa kihistoria uliojengwa juu ya misingi ya ushirikiano katika nyanja za kiuchumi na kijamii, huku Tanzania ikiendelea kuwa mdau muhimu wa maendeleo ya Taifa hilo.
Ziara ya Rais Dkt. Samia nchini Comoro inadhihirisha dhamira ya dhati ya Tanzania ya kuendeleza ushirikiano wa karibu wa kidugu, kihistoria na kidiplomasia na nchi hiyo pamoja na kuunga mkono juhudi za maendeleo na mshikamano wa nchi hiyo katika miaka 50 ya uhuru wake