BAADA ya klabu ya soka ya Simba kufungwa mabao 2-1 na Azam FC kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Kagame jana usiku, kocha wa Simba, Masoud Djuma, amesema mashabiki hawatakiwi kulalamika kwa kutokuwepo baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza.
Masoud ameyasema hayo kufuatia baadhi ya mashabiki waliokuwepo uwanjani kuonyesha kutoridhishwa na kiwango cha wachezaji waliopewa nafasi ambao wengi wao ni wale waliosajiliwa katika kipindi hiki cha usajili huku wachezaji wazoefu wakiachwa.
”Simba ina wachezaji 30, wengi wao wamecheza ligi na imeisha hawajapumzika, ikaja michuano ya SportPesa Super Cup kisha ikaja michuano hii ya CECAFA, mimi nikaamua wapumzike ili warudi kwenye ligi wakiwa vizuri na ninaamini itakuwa hivyo”, amesema.
Aidha ameongeza kuwa wachezaji wapya na wale ambao hawakupata nafasi kwenye ligi msimu uliopita ambao amewatumia kwenye michuano ya CECAFA, wameonyesha kiwango kikubwa na sasa anaweza kuamini ana kikosi kipana kwa ajili ya michuano mbalimbali msimu ujao.
Endapo Simba ingetwaa ubingwa jana ingekuwa ni mara yake ya saba kwani tayari ni mabingwa mara sita, wakishikilia rekodi ya kuchukua kombe hilo mara nyingi zaidi. Kwa upande wa Azam FC wao wametetea ubingwa wao ambao waliuchukua mwaka 2015 hivyo kuutwaa mara mbili.
Masoud Djuma ambaye ni raia wa Rwanda anaifundisha Simba kama kaimu kocha mkuu, baada ya aliyekuwa kocha mkuu, Pierre Lechantre, kumaliza mkataba na klabu hiyo mapema mwezi Juni na kurejea nyumbani kwao Ufaransa.
0 Comments:
Post a Comment