Friday, 13 July 2018

Fei Toto ni mali halali ya Yanga

Baada ya mchezaji Feisal Salum Abdalah maarufu 'Fei Toto' wa mabingwa wa soka visiwani Zanzibar JKU, kusaini timu mbili za Singida United na Yanga hapo jana, hatimaye JKU wameeleza kwanini nyota huyo alifanya hivyo.

Akiongea na www.eatv.tv Katibu mkuu wa JKU, Saadu Maalim Ujudi, ameweka wazi kuwa kilichotokea mpaka mchezaji Feisal Salum kuonekana akisaini timu mbili ndani ya siku moja ni kutokana na timu ya Singida United kutolipa ada ya kuvunja mkataba wa mchezaji huyo na JKU.

''Singida United walitaka kumsajili Feisal Salum wakaja tukaongea na tukakubaliana lakini wakaenda bila kulipa pesa ya kuvunja mkataba na jioni Yanga wakaja na hela kamili na sisi tulitaka timu ije na hela kamili hatukutaka maneno kwahiyo tukachukua pesa yetu naye akasaini'', amesema.

Aidha Saadu amesema Singida United walipaswa kuvunja kwanza mkataba wa miaka miwili aliokuwa nao Feisal ndani ya JKU lakini hawakufanya hivyo, badala yake wakampa pesa binafsi tu kwahiyo walielewana Yanga watawarudishia Singida United pesa yao ndio maana mchezaji huyo akasaini Yanga.

Mapema jana Julai 12, 2018, klabu ya Singida United ilitangaza kumsajili kiungo Feisal kwa mkataba wa miaka mitatu lakini baadaye jioni Yanga nao wakamtambulisha mchezaji huyo wakimsainisha mkataba wa miaka mitatu pia.

EATV

0 Comments:

Post a Comment