Friday, 13 July 2018

Hatima ya viongozi wa CHADEMA kujulikana Julai 20


Hatima ya maombi ya viongozi wa Chadema  wanaokabiliwa kesi ya jinai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, itajulikana Julai 20, 2018 baada ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi wa pingamizi la Serikali.

Viogozi hao wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe  wamefungua maombi ya mapitio Mahakama Kuu  dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), wakipinga uamuzi na amri mbalimbali zilizotolewa na Mahakama ya Kisutu katika kesi hiyo.

Wameiomba Mahakama Kuu kuitisha jalada la kesi hiyo kutoka Kisutu ili kuchunguza na kujiridhisha na usahihi na uhalali wa amri hizo.

Hata hivyo DPP amewasilisha pingamizi la awali dhidi ya maombi hayo,  akiiomba mahakama hiyo iyatupilie mbali kwamba madai yao  ni batili kwa kuwa yanakiuka Sheria ya Mahakama za Hakimu Mkazi, kifungu cha 43 (2).

Pingamizi hilo la awali limesikilizwa jana  Ijumaa Julai 13, 2018 na Jaji Rehema Sameji ambaye baada ya kusikiliza hoja za pande zote, amepanga kutoa uamuzi Julai 20,2018.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Wilbard Mashauri ni Katibu Mkuu, Dk Vicent  Mashinji; naibu makatibu wakuu John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Wengine ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa;  mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; mbunge wa Kawe, Halima Mdee; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Wote wanakabiliwa na  mashtaka 13, ambayo ni kufanya mikusanyiko na maandamano yasiyo halali, yanayaowakabiliwa washtakikwa wote huku Mbowe, Mchungaji Msigwa, Mdee na Heche kila mmoja akikabiliwa na mashtaka zaidi.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 112, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 16, 2018 katika barabara ya Kawawa, Mkwajuni Kinondoni na kusababisha vurugu zilizosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline.

0 Comments:

Post a Comment