Wednesday 18 July 2018

Kesi ya vigogo CHADEMA yakwama tena

Kesi ya kufanya mikusanyiko na maandamano yasiyo halali, inayowakabili viongozi tisa wa Chadema, akiwamo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, imeshindwa kuendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kesi hiyo imeshindwa kuendelea leo Julai 18, kwa sababu upande wa mashtaka wanasubiri uamuzi wa maombi yaliyowasilishwa Mahakama Kuu, na washtakiwa hao.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa ili kusubiri maamuzi ya maombi yaliyopelekwa Mahakama Kuu.

Nchimbi akisaidiana na Wakili Zainabu Mango na Saimon Wankyo, alidai kuwa maombi ya awali yaliyowasilishwa Mahakama Kuu, yalisikilizwa wiki iliyopita na kupangiwa Julai 20, kwa ajili ya kutolewa maamuzi hivyo wanaomba ipangwe tarehe ya karibu kwa ajili ya kusubiri maamuzi yatakayotolewa.

Hata hivyo, wakati kesi hiyo inatajwa jana, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, hakuwepo mahakamani hapo kutokana na kuuguliwa na mke wake ambaye amelazwa katika Hospitali ya Bugando.

"Kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa tunasubiri uamuzi wa maombi yaliyowasilishwa Mahakama Kuu, na washtakiwa hawa," alidai Nchimbi.

Nchimbi baada ya kueleza hayo, Wakili wa utetezi Peter Kibatala akisaidia na Jeremiah Mtobesya, alidai kuwa mapingamizi ya awali yameshatolewa, hivyo wanaomba mahakama iendelee kuitaja kesi hiyo.

"Ni kweli John Heche hayupo mahakamani hapa na nimepata taarifa kutoka kwa mdhamini wake, kuwa   anauguliwa na mke  wake, lakini mdhamini wake anazo fomu za matibabu,  ataziwasilisha hapa mahakamani," alisema Kibatala.

Kibatala alifafanua kuwa kama mapingamizi hayo yatafanikiwa basi kesi itapangwa kwa ajili ya kusikiliza na kama hayatafanikiwa itaendelea kupangwa kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya mdhamini huyo kuwasilisha fomu hizo mahakamani hapo, upande wa mashtaka walidai kuwa hawana pingamizi juu ya uthibitisho huo wa matibabu.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 25, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Viogozi hao wa Chadema, wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe walifungua maombi ya mapitio Mahakama Kuu dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), wakipinga uamuzi na amri mbalimbali zilizotolewa na Mahakama ya Kisutu katika kesi hiyo.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu, Dk Vincent Mashinji; naibu makatibu wakuu John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Wengine ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; mbunge wa Kawe, Halima Mdee; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 112 ya mwaka 2018, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 16, 2018 katika barabara ya Kawawa, Mkwajuni Kinondoni ambalo wanadaiwa kusababisha vurugu zilizosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline

0 Comments:

Post a Comment