KIKOSI cha Simba SC kinatarajiwa kuondoka Dar es Salaam Ijumaa kwenda Uturuki kuweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya.
Habari ambazo kutoka Simba SC zimesema kwamba wachezaji wote waliosajiliwa watasafiri kwa kambi hiyo.
Na ikiwa huko, Simba SC ambayo kwa sasa inaongozwa na Kaimu Kocha Mkuu, Mrundi Masoud Juma baada ya kuondoka kwa Mfaransa, Pierre Lechantre itacheza mechi za kirafiki pia za kujipima nguvu.
Na taarifa zaidi zinasema kwamba huko Uturuki ndiko kocha mpya mtarajiwa, Mbelgiji Patrick Winand J. Aussems ataanzia kazio.
Kocha huyo aliyezaliwa Februari 6, mwaka 1965 mjini Moelingen, Ubelgiji ana uzoefu wa kufundisha timu kadhaa Asia na Ulaya – lakini amewahi kufundisha KSA ya Cameroon na AC Leopards ya Dolisie nchini Kongo, hizo zikiwa timu pekee za Afrika.
Aussems alikuwa Dar es Salaam mapema mwezi huu kwa mazungumzo ambayo inasemekaana yamekwenda vizuri na ataapewa kazi Msimbazi.
Aussems alianza kama mchezaji wa kwao, akichezea klabu za RCS Vise (1974–1981), Standard Liege (1981–1988), K.A.A. Gent (1988–1989), R.F.C. Seraing (1989–1990) na ES Troyes AC ya Ufaransa kuanzia mwaka 1990 hadi 1993, ambayo ilikuwa timu yake ya kwanza kufundisha akianza kama kocha mchezaji mwaka 1992.
Mwaka 1995 alienda kufundisha SS Saint-Louisienne hadi 1999 alipohamia Capricorne Saint-Pierre hadi 2002 alipokwenda Stade Beaucairois hadi 2003 alipojiunga na Stade de Reims zote za Ufaransa hadi mwaka 2004 alipokuja Afrika kufundisha KSA ya Cameroon hadi mwaka 2006 aliporejea Ufaransa kufundisha SCO Angers.
Timu nyingine alizofundisha ni Evian Thonon Gaillard F.C. ya Ufaransa pia kuanzia 2009 hadi 2011 alikwenda China kufundisha Shenzhen Ruby (2011) na Chengdu Blades kuanzia 2012 hadi 2013 aliporudi Afrika kufundisha AC Leopards hadi mwaka 2015 alipokwenda kufundisha timu ya taifa ya Nepal.
Kwa upande wake, Lechantre aliyekuja na msaidizi wake binafasi Simba, Mtunisia Aymen Hbibi Mohammed aliondokea nchini Kenya mwezi uliopita timu ilipokuwa kwenye michuano ya SportPesa Super Cup, baada ya kutofautiana na uongozi.
Lechantre aliyeanza kazi Januari 18 tu, mwaka huu ghafla alisusa kazi nchini Kenya baada ya mechi moja dhidi ya Kariobangi Sharks na akapanda jukwaani wakati Simba SC ikimenyana na Kakamega Homeboyz katika Nusu Fainali ya SportPesa Super Cup na kuibuka na ushindi wa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Afraha pia.
Timu iliongozwa na Kocha Msaidizi, Mrundi Masoud Juma aliyekaa benchi na kocha wa makipa, Muharami Mohammed ‘Shilton’ hadi kufika fainali ambako ilifungwa na Gor Mahia.
Na ni makocha hao pia walioiongoza Simba SC hadi kufika fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashafriki an Kati, Kombe la Kagame ambako ilifungwa 2-1 na Azam FC.
0 Comments:
Post a Comment