Kuna wakati unaweza ukawa unashangaa kwa nini ndoto zako hazitimii? Utakuta umejiwekea malengo yako vizuri, lakini unashangaa ni malengo machache sana yanayotimia au wakati mwingine hakuna kabisa.
Sina shaka yoyote umeshawahi kukutana na hali kama hii wakati fulani katika maisha yako. Kiuhalisia, yapo mambo mawili ambayo kitaalamu hupelekea ndoto zako kushindwa kutimia ikiwa hutayajua vizuri.
Jambo la kwanza, ni kutokujua kile unachokitaka vizuri. Hili ni jambo ambalo hupelekea wengi kushindwa kufanikisha ndoto zao kabisa. Kama hujui kile unachokitaka vizuri, suala la kufanikisha ndoto zako litakuwa gumu kidogo.
Katika akili yako ili uweze kufanikisha ndoto yako au jambo unalolitaka kwa urahisi, ni lazima kile kitu unachokitaka uweze kukijua vizuri. Tambua njia utakazotumia hadi kukipata kitu hicho pia tambua kitu hicho changamoto zake ni zipi.
Acha kufanya kosa la kuuchanganya ubongo wako kwa kuupa vitu vingi. Kuwa maalumu kwa kujua vizuri kile unachokitaka. Usipojua kile unachokitaka kwa uhakika na kukifanyia kazi, ni wazi hutaweza kufanikiwa na hilo halina ubishi.
Jambo la pili, ni kukosa hamasa ya kutosha kwa kitu hicho unachokitaka. Hamasa ni kitu cha muhimu sana ili kufikia ndoto zako. Ukishakijua kitu hicho vizuri, hamasa itakusaidia kufanya kila jitihada hata kama umechoka.
Wengi ni watu wa kutaka kufikia lengo fulani katika maisha yao, lakini kwa bahati mbaya hujikuta ni watu wa kukosa hamasa ya kuwasukuma kuweza kukamilisha malengo yao.
Ili kufanikiwa, fanya kila ufanyalo kuhakikisha una hamasa ya kufanya hicho unachotaka kukifanya katika maisha yako. Inapotokea hamasa hiyo umeikosa acha kusimama eti kwa sababu ya kukosa hamasa.
Maisha hayasimami eti kwa sababu wewe hujisikii kufanya kitu fulani au umekosa hamasa. Endelea kusonga mbele, huku ukitafuta hamasa ya kufanikiwa kwako kila siku. Ukifanya hivyo utafika mbali kimafanikio.
Katika hali ya kawaida, kama kila wakati unakosa mambo haya mawili suala la kufanikiwa kwako linakuwa ni gumu sana. Hivyo, ni lazima sana kwako kujua vizuri kile unachokitaka na kuwa na hamasa kubwa yaani ‘burning desire’ ya kuhakikisha kitu hicho ni lazima unaweza kukipata.
Ukichunguza watu wengi ambao hawajafanikiwa wanashindwa kufanikiwa kwa sababu hizi mbili tu na si vinginevyo. Kama unafikiri natania anza kufatilia, huku lakini ukianza na wewe.
Kama unajiona hujafanikiwa vya kutosha jiulize binafsi je, unakijua vizuri kile unachokitaka na huna tamaa ya kutaka hiki mara kile na mwisho wa siku kuwa na malengo mengi yasiyotekelezwa?
Usiishie hapo tu, tena kama unaona hujafanikiwa vya kutosha jiulize, je, una hamasa kubwa ya kuona ndoto zako zinatumia? Je, unakosa usingizi na kuamua kujituma usiku na mchana hadi kufanikiwa?
Ukipata majibu ya maswali hayo yatakusaidia sana kuweza kufanikiwa na kuwa mtu mwingine tofauti na hatimaye kuweza kufanikisha zoezi zima la kutimiza ndoto zako. Jitoe kikamilifu kuona ndoto zako zinatimia kwa kuyajua mambo hayo mawili.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
0 Comments:
Post a Comment