Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Bodi ya Ligi (TPLB) limetangaza ratiba ya awali ya Ligi Kuu Bara kwa ajili ya msimu wa 2018/19.
Ligi hiyo inatarajiwa kuanza Agosti 22 kwa michezo kadhaa kupigwa.
Mabingwa wa Tanzania Bara, Simba watashuka dimbani siku ya ufunguzi kupepetana na Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Taifa.
Michezo hiyo ya ufunguzi, itatanguliwa na mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Simba dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Agosti 18 2018.
Mbali na mchezo wa Simba dhidi ya Prisons, ratiba hiyo inaonesha mechi nyingine zitakazoanza Agosti 22 ni kati ya Ruvu Shooting dhidi ya Ndanda FC, Singida United United dhidi ya Biashara FC pamoja na Kagera Sugar watakaocheza na Mwadui FC.
Yanga watashuka dimbani August 23 kucheza na Mtibwa Sugar.
Mchezo wa kwanza wa watani wa jadi, Simba na Yanga utapigwa Septemba 30, Simba ikiwa mwenyeji.
Ligi hiyo itahusisha jumla ya mechi 380 kutoka 240 ambazo zilichezwa msimu uliopita kutokana na ongezeko la timu.
Jumla ya timu 20 zitashiriki ligi kuu msimu ujao ikiwa ni ongezeko la timu nne zaidi ya msimu uliopita.
Kila timu itacheza michezo 38.
Ratiba kamili itawekwa kwenye ukurasa wa ratiba.
0 Comments:
Post a Comment