WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva usiku wa Jumanne ametokea benchi timu yake, Difaa Hassan El Jadida ikikamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza Kundi B Ligi ya Mabingwa Afrika bila ushindi, baada ya kuchapwa mabao 2-1 na wenyeji, ES Setif Uwanja wa Mei 8, 1945 mjini Setif nchini Algeria.
Wachezaji wa Difaa El Hassan El Jadida watajilaumu wenyewe kwa kipigo hicho, kwani baada ya sare ya 1-1 kwa muda mrefu, wakawaruhusu wenyeji kupata bao la ushindi dakika za mwishoni kabisa za mchezo.
Ali Bamaamar alianza kuifungia Difaa Hassan El – Jadida dakika ya nne, kabla ya Habib Bouguelmouna kuisawazishia ES Setif dakika ya 21.
Msuva akaingia uwanjani dakika ya 64 kwenda kuchukua nafasi ya Chouaib El Maftoul na Setif wakapata bao la ushindi dakika ya 89 kupitia kwa Houssameddine Guecha aliyetanguliwa pasi nzuri na Samir Aiboud aliyeingi uwanjani dakika ya 65 kuchukua nafasi ya Akram Djahnit.
Mapema katika mechi nyingine ya kundi hilo iliyotangulia, bao la dakika ya 88 la Meshack Elia aliyetokea benchi dakika ya 63 kuchukua nafasi ya Ben Malango Ngita lilitosha kuwapa wenyeji, TP Mazembe ushindi wa 1-0 dhidi ya MC Alger ya Algeria.
Kwa matokeo hayo, Mazembe inaendelea kuongoza Kundi B kwa pointi zake tisa baada ya kushinda mechi zake zote tatu, ikifuatiwa na MC Alger yenye pointi nne, Setif pointi tatu na Jadida pointi moja mkiani.
Kikosi cha ES Setif kilikuwa; Moustapha Zeghba, Saadi Redouani, Miloud Rebai, Abdelkader Bedrane, Houari Ferhani, Akram Djahnit/Samir Aiboud dk65, Ilyes Sidhoum, Mohamed Bakir/ Mustapha Boussif dk77, Abdelmoumene Djabou, Houssameddine Guecha na Habib Bouguelmouna/Hamza Banouh dk90+3.
Difaa Hassan El Jadida; Mohamed El Yousfi, Tarik Asstati, Marouane Hadhoudi, Youssef Aguerdoum, Saad Lagrou, Chouaib El Maftoul/Simon Msuva dk64, Anouar Jayid, Mohamed Ali Bamaamar, El Mehdi Karnass, Adnane El Ouardy/Anthony Okpotu dk71 na Ayoub Nanah/Bilal Megri dk81.
MATOKEO YA MECHI ZOTE NA MISIMAMO YA MAKUNDI GONGA HAPA KUTAZAMA
0 Comments:
Post a Comment