Sunday 12 August 2018

Mawenzi Market 0-1 Yanga

BAO pekee la mshambuliaji mpya, Haritier Makambo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) limeipa ushindi wa 1-0 Yanga SC dhidi ya Mawenzi Market katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. 
Huo unakuwa ushindi wa kwanza wa Yanga SC ndani ya mechi sita, tangu iliposhinda mara ya mwisho Jumanne ya Mei 22 bao 1-0 dhidi ya Mbao FC, bao pekee la kiungo Mzimbabwe, Thabani Scara Kamusoko aliyemtungua kwa shuti la mpira wa adhabu, kipa wa mkopo Metacha Boniphace Mnata kutoka Azam FC dakika ya 26. 

Baada ya hapo, ilitoa sare mchezo uliofuata wa Ligi Kuu 2-2 na Ruvu Shooting FC Uwanja wa Taifa kabla ya kwenda kufungwa mechi nne mfululizo, 3-1 na Azam FC Ligi Kuu Taifa, 3-1 na Kakamega Homeboyz FC Nakuru nchini Kenya michuano ya SportPesa Super Cup, kabla ya kufungwa mara mbili mfululizo na Gor Mahia 4-0 mjini Nairobi na 3-2 Dar es Salaam Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika. 
Mchezo wa leo ulikuwa maalum wa kumuaga aliyekuwa Nahodha wa klabu kwa muda mrefu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye baada ya kuitumikia klabu tangu mwaka 2006, sasa anakuwa Meneja wa timu. 
Cannavaro alicheza kwa dakika 10 tu kabla ya mchezo kusimama kumpa fursa ya kuaga na kukabidhi beji kwa Nahodha mpya, Kelvin Yondan na jezi yake, namba 23 kwa Abdallah Shaibu ‘Ninja’. 
Baada ya mchezo huo, Yanga SC itaendelea na kambi yake mjini Morogoro pamoja na kujiandaa na msimu mpya, lakini pia mchezo wake ujao wa Kombe la Shirikisho dhidi ya USM Alger Agosti 19 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 

0 Comments:

Post a Comment