Tuesday 30 May 2023

Dili La Beki Kutua Simba Lafikia Patamu

Kama ulikuwa unadhani Simba imelala baada ya kushindwa kutwaa taji lolote kwa msimu wa pili mfululizo, basi umekosea kwani tayari mabosi wa timu hiyo wapo bize kusaka vifaa vya msimu ujao akiwemo beki wa timu ya taifa ya Rwanda, Thierry Manzi aliyethibitishia kuwa anakuja bongo.
Beki huyo ambaye ni nahodha msaidizi wa Amavubi, alisema kuwa yupo njiani kuja Tanzania kwa ajili ya kumalizana na Simba. Manzi aliyezipa mataji mbalimbali timu za APR na Rayon Sports za Rwanda kwa vipindi tofauti, hivi karibuni alikuwa Ubelgiji alikoenda kuzungumza na baadhi ya timu zilizotaka kumsajili, lakini sasa amebadili gia hewani na atarudi nchini kwao kisha kuja Tanzania kuzungumza na mabosi wa Simba.
“Kama kila kitu kitakuwa sawa nitakuja Tanzania kuzungumza na timu lakini kwa sasa nikitoka huku (Ubelgiji) nitaenda kwanza nyumbani Rwanda,” alisema Manzi.
Beki huyo ni miongoni mwa wachezaji waliopendekezwa Simba na Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’, anayeamini atamfaa kikosini hapo kwani waliwahi kufanya kazi pamoja miaka kadhaa nyuma wakiwa kikosi cha Rayon Sports kabla ya Robertinho kutimkia Gor Mahia ya Kenya na Manzi kwenda FC Dila ya Geogia, kisha FAR Rabat ya Morocco kabla hajavunja mkataba na kurejea AS Kigali ya Rwanda.
Aidha nyota mwingine aliyependekezwa na Robetinho ni winga Mcameroon Leandre Onana anayeongoza kwa ufungaji wa mabao kwenye Ligi Kuu ya Rwanda akifunga mara 15 akiwa na timu yake ya Rayon Sports sambamba na kuasisti mara sita.
Inafahamika kuwa Meneja wa Onana ndiye meneja wa Robertinho, hivyo huenda dili hilo likakamilika mara tu staa huyo wa Rayon atakapomaliza msimu akiwa amebakiza mechi moja ya mwisho ya ligi dhidi ya Sunrise itakayopigwa leo na fainali ya michuano ya ‘Peace Cup’ dhidi ya APR mapema mwezi ujao.
Hata hivyo, inaelezwa mabosi wa Simba nao wameshusha wachezaji wao katika maeneo tofauti tofauti na wale aliowapendekeza Robertinho na tayari wapo Dar es Salaam wakisuburi makubaliano ya pande zote mbili ili wasaini mkataba. Simba inataka kurejesha ufalme ilioupoteza kwa misimu miwili sasa na ili kuhakikisha hilo imepanga kusajili wachezaji bora ambao wataifikisha nchi ya ahadi.
Pia tayari matajiri hao wa Msimbazi wameanza mazungumzo ya kuhakikisha inawabakiza mastaa wake muhimu kikosini na kuachana na wengine wengi ambao hawawahitaji.
Beno Kakolanya, Gadiel Michael, Mohamed Ouattara, Ismail Sawadogo, Augustine Okrah na Peter Banda ni miongoni mwa wachezaji ambao huenda wakaondoka Simba mwishoni mwa msimu huu.
Wakati hayo yakiendelea, Simba imeendelea kujifua kwenye uwanja wake wa Mo Simba Arena ikijiandaa na mechi mbili za kuhitimisha Ligi itakazocheza jijini Dar dhidi ya Polisi na Coastal Union.

0 Comments:

Post a Comment