Saturday, 27 May 2023

Hizi Hapa Kazi Tano Za Daalder Simba


JUZI mchana Simba ilimtangaza Mholanzi, Mels Daalder kuwa skauti wake mkuu ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kuwa na mtaalamu rasmi katika eneo hilo.

Daalder nje ya kuwa mtaalamu wa skauti lakini pia ni mjuzi wa kufanya uchambuzi (analysis), pia ana uzoefu mkubwa wa ligi ya Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika kiujumla na katika miaka ya hivi karibuni alijinasibu kama shabiki wa Simba na mara kadhaa alionekana amevaa jezi za Simba na wakati mwingine akipiga picha na wachezaji mbalimbali wa Tanzania na nchi nyingine.

Mels mwenye uzoefu wa kufanya skaunti duniani ameshiriki kozi mbalimbali za kazi hiyo ikiwa ni pamoja na zile zilizoendeshwa na mkuu wa skaunti wa zamani wa Manchester United, David Hobson.

Ujio wa Daalder ndani ya Simba utakuwa na mabadiliko chanya katika maeneo mengi lakini kubwa ni kwenye usajili na hizi ni kazi tano ambazo atazifanya akiwa Simba.

Mosi ni kutafuta na kupendekeza wachezaji kwa benchi la ufundi la Simba. Hii ni kazi ya kwanza kwa Daalder hususani katika nyakati hizi za usajili wa dirisha kubwa.

Mtaalamu huyu atakuwa na kibarua cha kupitia ripoti ya benchi la ufundi la Simba na kuangalia aina ya wachezaji wanaohitajika kisha kupendekeza nani na nani wanafaa katika eneo flani.

Pili atalisaidia benchi la ufundi kutambua ubora wa wachezaji wao. Mfano kwa sasa Simba inampango wa kuachana na wachezaji zaidi ya watano lakini kati yao huenda wapo walioonewa na wengine walistahili.

Uwepo wa Daalder Simba utalisaidia benchi la ufundi kuchambua na kujua ubora halisi wa wachezaji wao aina yao ya uchezaji na namna ya kuwatumia.

Tatu ni kupunguza upigaji watu wengi kwenye usajili. Sio jambo geni kwa timu za Tanzania ikiwemo Simba kusajili wachezaji wasio stahili na hii mara nyingi ni kutokana na kutokuwa na mtu maalumu wa kufuatilia mienendo ya wachezaji wa timu pinzani wanaohitajika. Jukumu la kuchagua na kupendekeza wachezaji kwa sasa litakuwa kwa Daalder na benchi la ufundi na sio viongozi wenye maslahi yao binafsi na kama watampa uhuru basi huenda upigaji ukapungua.

Nne ni kuipa Simba machaguo mengi katika usajili. Hii ni faida nyingine ya kuwa na mtaalamu huyu pale Msimbazi, kutokana na kazi yake kuwa ya kuangalia na kutathimini ubora wa wachezaji katika timu nyingine na maeneo mengine basi ataipa Simba machaguo mengi ya usajili endapo itahitaji kufanya hivyo.

Daalder atakuwa anazunguka sehemu mbalimbali kufuatilia muenendo wa wachezaji tofauti hivyo mfano timu inataka winga atakuwa na uwezo wa kuleta mezani mawinga wengi zaidi na kuainisha kila sifa ya kila mmoja wao, ubora na udhaifu wao na kisha benchi la ufundi kuchagua ni yupi atawafaa.

Tano na mwisho kwa leo ni kupunguza matumizi ya fedha katika usajili. Kazi ya Daalder pia inahusika kwenye kuangalia wachezaji vijana au chipukuzi katika timu za vijana za klabu, timu nyingine na hata mtaani hivyo kama katika ziara zake atapata mchezaji mzuri basi anaweza kuirahisishia timu kumpata kwa gharama nafuu kuliko kwenda sokoni kutafuta mchezaji wa bei ghali ambaye unakuta ubora wake ni sawa na yule wa kawaida.

Akizungumza juu ya uteuzi huo Ofisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Imani Kajula alisema “Tunafuraha kubwa kumkaribisha Mels ili kuja kuboresha ufanisi kwenye skautingi kwani ni eneo muhimu sana kwenye mafanikio ya klabu yetu. Tunaendelea na maboresho muhimu kuelekea msimu mpya wa ligi na mashindano ya kimataifa”.

0 Comments:

Post a Comment