Mwanza. Kenny na Lenny Makomonde (24), mapacha na wanafunzi wa Chuo cha Mipango Kampasi ya Mwanza wamefariki dunia kwa kuzama majini walipokuwa wakiogelea ndani ya Ziwa Victoria.
Tukio hilo lililoacha simanzi na vilio miongoni mwa wanafunzi wa chuo hicho, ndugu, jamaa na marafiki limetokea jioni ya Mei 28, 2023 wakati wawili hao walipokuwa wakiogelea kwenye ufukwe wa Mihama Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
Miili ya mapacha hao wanaosemekana kuwa na ujuzi na uzoefu wa kuogelea tayari imepatikana na kuopolewa kutoka majini na Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakishirikiana na wananchi.
Mkuu wa Jeshi la Zima Moto Wilaya ya Ilemela, Insekta Deusdedith Rutta amesema taarifa za mapacha hao waliokuwa wanasoma kozi ya Mipango na Maendeleo kuzama maji ziliifikia Jeshi hilo Saa 1:00 usiku jana Mei 28, 2023.
‘’Juhudi za uokoaji zilishindikana kutokana na kiwazo cha giza,’’ amesema Inspekta Rutta
Amesema askari wa Zimamoto na Uokoaji walirejea eneo la tukio leo alfajiri kuendelea na uokoaji na kufanikiwa kuopoa miili ya mapacha hao Saa 5:00 asubuhi.
Baba mzazi wa mapacha hao, Makomonde Deus amesima vifo vya watoto wake ni pigo na vimeacha simanzi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa sababu vimetokea ghafla.
“Hatuna la kufanya kwa sababu tunaamini ni mpango wa Mungu. Watoto wangu walikuwa wazefu wa kuogelea na mara kwa mara wanaogelea kila wanapopata nafasi. Kilichotokea ni mipango ya Mungu,’’ amesema Makomonde
Mmoja wa wanafunzi aliyekuwa anasoma darasa moja na mapacha hao aliyejitambulisha kwa jina la Andrew Sengeo amesema vifo vivyo ni pigo na vimeacha simanzi miongoni mwa wanafunzi kutokana jinsi marehemu hao walivyokuwa na ushirikiano na wengine enzi za uhai wao.
Ibada ya kuaga miili ya mapacha hao inaendelea eneo la Chuo cha Mipango kampasi ya Mwanza na juhudi za kupata kauli za viongozi wa chuo hicho kuzungumzia tukio hilo zinaendelea.
0 Comments:
Post a Comment