Monday 29 May 2023

Sekta Ya Elimu Yaongoza Tuhuma Za Rushwa

Mtwara. Sekta ya elimu yaongoza kutuhumiwa kuwa na malalamiko ya rushwa mkoani Mtwara kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (Takukuru) mkoani hapa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi, 2023.

Mkuu wa Takukuru mkoani Mtwara, Enock Ngailo amesema hayo jana Jumatatu Mei 29, 2023 kuwa katika malalamiko 27 yanayohusu rushwa waliyoyapokea manne yapo katika sekta ya elimu.

Amesema sekta za afya, Utawala, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na ushirika kila moja ina tuhuma tatu zikifuatiwa na ardhi, uchukuzi na kilimo zenye tuhuma mbili kila moja.

Aidha sekta za mahakama, polisi, Msalaba mwekundu, usajili wa vizazi na vifo, (Rita) na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, (Nida) vikiwa vimelalamikiwa mara moja moja.

Ngailo amesema uchunguzi unaendelea ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo.

Katibu wa Chama cha Walimu, (CWT) Mkoa wa Mtwara, Rashid Mchekenje ameiomba Takukuru kuendelea kufatilia hasa katika maeneo ya upandishwaji wa vyeo kwa walimu wakuu, wakuu wa shule na maafisa elimu kata.

“Usimamizi wa mitihani ndio unalalamikiwa sana wanaochaguliwa ni wale wale kila mara inaleta malalamiko sana wangekuwa wanabadilishana,” Mchekenje ameiambia Mwananchi Digital na kuongeza.

“Mengine tunayoyapata ni masuala ya uhamisho wengine wanalipwa kwa upendeleo wengine hawalipwi hadi mtu ajiongeze,” amemalizia.

0 Comments:

Post a Comment