Monday, 29 May 2023

Simba Ilifeli Kwenye Usajili

MIAKA inakwenda sana. Nyakati zinabadilika sana, kila kitu kilivyokuwa jana leo kimebadilika, ndio maisha ya mwanadamu.

Nani aliwaza kuwa leo hii tungekuwa tunatumia simu janja na sio viswaswadu? Hakuna. Dunia ilikuwa gizani, nani anakumbuka zile kompyuta zilizokuwa na uchogo nyuma kama bodi la Scania?

Nyakati zile tuliona kama kifaa cha maana, lakini leo hii watu wanatembea na kompyuta zikishikiliwa  mkononi. Inafurahisha sana.

Nyakati kwenye soka nazo zinakwenda kwa kasi ya ajabu. Ukiwagusa watu wa zamani watakwambia kuhusu Makumbi Juma, Sunday Manara, Zamoyoni Mogella na wengineo. Lakini leo tunajivunia Mbwana Samatta. Ndiye staa wa nyakati hizi.

Nyakati za hapa karibuni nazo zimebadilika kwa kasi. Kulikuwa na ubabe wa Yanga ya Yusuf Manji ulitawala soka la Bongo kama ilivyojisikia.

Ni katika nyakati hizi Yanga ilibeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara kisha ikabeba tena. Ilikuwa na wachezaji waliotisha. Nani anamkumbuka Haruna Niyonzima katika ubora wake? Angefanya anachojisikia pale kwa Mkapa. Nani anawakumbuka kina Donald Ngoma, Saimon Msuva na Amissi Tambwe? Walifunga walivyojisikia.

Nyakati zikabadilika. Ikaja Yanga ya kubeba bakuli. Ilikuwa na maisha magumu kuliko ugumu wenyewe, walitia huruma ndanina nje ya nchi.

Timu ikasajili wachezaji wa ovyo kama kina Yikpe, Bigirimana na wengineo. Mchezaji hata kutuliza mpira ni tabu lakini wangefanya nini? Huu ndio ulikuwa uwezo wa timu yao.

Ndio nyakati ambazo Simba ikautwaa ufalme wa soka letu. Ikashusha vifaa vya maana kutoka ndani na nje ya nchi. Mchezaji wa maana kama Meddie Kagere akatua Simba. Nani alitegemea? Kagere alikuwa anafunga kama vile amezaliwa golini.

Wakashusha wachezaji wanyumbulifu kama Clatous Chama na Luis Miquissone. Waliishi katika dunia yao ilifika hatua watu wanajiuliza mchezaji huyu amewezaje kucheza timu yaTanzania? Lakini Simba waliweza kwa jeuri ya fedha za Mohamed Dewji.

Wakatua pale Chamazi na kuchukua wachezaji wote wa maana wa Azam FC. Nani aliwaza kama nyakati zingekuja kina John Bocco, Aishi Manula, Shomary Kapombe na wengineo wangeweza kucheza Simba? Hakuna. Hata uwe Mganga wa Kienyeji kutoka Sumbawanga usingeweza kutabiri.

Simba ikatawala soka la hapa ikatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo, ikabeba taji la FA na mengine mengi. Ilifanya kile ilichojisikia.

Huko Afrika Simba ikafika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa mara mbili. Nani aliwaza kuwa timu ya Tanzania ingeweza kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa mara mbili ndani ya miaka mitatu? Simba wakafanya ionekane kama kazi nyepesi.

Nyakati zimekwenda wapi? Simba sasa inamaliza msimu wa pili bila kubeba taji lolote la maana. Ni Simba ile ile chini ya Dewji. Kama ni fedha bado anazo kama ni Kambi bado wanakaa sehemu za maana. Kama ni posho bado wanalipwa nyingi. Nini kimebadilika? Subiri nitakueleza.

Katika misimu hii miwili Simba imefeli zaidi katika usajili wa wachezaji. Tazama lundo la wachezaji waliokuja na kuondoka ndani ya muda mfupi wakiwa hawajafanya lolote la maana.

Msimu uliopita walisajiliwa kina Duncan Nyoni, Yusuph Mhilu, Peter Banda na wengineo. Wamefanya nini cha maana? Hakuna. Wengine waliondoka ndani ya muda mchache tu waliobaki hakuna jipya wanalofanya hadi sasa.

Msimu huu mambo ndio yamekuwa ovyo zaidi, wakasajili hadi Mzungu lakini hakuwa na jipya. Unajiuliza Mzungu anawezaje kuja kucheza Manungu, Mkwakwani, Ilulu, Ushirika na kwingineko. Ni uongo mtupu.

Wakamsajili Victor Akpan kutoka pale Coastal Union ya Tanga, mchezaji mzuri wa kawaida. Amefanya nini? Hakuna. Wakaishia kumtoa kwa mkopo.

Vipi kuhusu Nelson Okwa na Mohamed Oattarra? Wachezaji fulani tu wa mchongo. Wamekuja lakini hawakuwa na jipya. Mchezaji anatoka Nigeria halafu ama Ghana lakini anashindwa kuingia kikosi cha kwanza cha Simba? Huku ndio kufeli kwenyewe.

Katika lundo la wachezaji waliosajiliwa Simba msimu huu ni Moses Phiri na Sadio Kanoute pekee walioonekana kuwa na jipya. Pia huyu Jean Baleke aliyetua katika drisha dogo. Mshambuliaji wa kweli anafunga karibu kila mechi.

Huyo Ismail Sawadogo alisajiliwa na nani? Ni kituko kingine ndani ya Simba, mchezaji fulani wa kawaida sana hadi unajiuliza amefikaje pale Msimbazi. Huku ndiyo kufeli kwa Simba msimu huu.

Hakuna sababu ya kutafuta mchawi. Simba hawako vizuri katika eneo la usajili, hawako makini tena. Tazama wachezaji waliotua Yanga kisha utazame wale wa Simba utaelewa vizuri, kuna mahali wanapaswa kurekebisha.

Sishangai kuona wameanza kwa kuajiri mtu wa kusaka vipaji. Hata hivyo pengine amekuja kwa kuchelewa lakini ni wazi kuwa Simba inapaswa kuweka nguvu kubwa katika kutafuta wachezaji wa maana.

Kama walivyowapata kina Chama, Miquissone, Bwalya, Kagere na wengineo kwa wakati ule, ndivyo wanapaswa kufanya sasa. Wakishindwa watakwenda msimu mwingine wa aibu. Nimekaa paleee nawatazama.


0 Comments:

Post a Comment