Tuesday 30 May 2023

Tume Yatua Kilimanjaro Uchunguzi Kifo Tata cha Mwanachuo Nusura

Tume Yatua Kilimanjaro Uchunguzi Kifo Tata cha Nusura
Moshi. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania (THBUB) imebisha hodi mkoani Kilimanjaro kufanya uchunguzi huru juu ya kiini cha kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), Nusura Abdalah.



Taarifa zilizopatikana jana zilisema tume hiyo iliwasili katika Mji wa Himo Mei 26 mwaka huu na kuhoji watu mbalimbali wakiwamo daktari na wauguzi wa Hospitali ya Faraja waliompokea Nusura na baadaye kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu.



Ingawa orodha ya waliohojiwa haijawekwa wazi, taarifa za uhakika kutoka vyanzo vya kuaminika kutoka Himo, zilisema tume ilimhoji pia anayedaiwa kuwa mchumba wa Nusura pamoja na dereva wa gari lilimbeba hadi hospitali.



Taarifa kutoka Hospitali ya Faraja zilizonukuliwa awali zikimkariri daktari Peter Minja aliyemhudumia Nusura, kuwa mwanafunzi huyo alifikishwa hospitalini hapo Mei mosi mwaka huu kati ya saa 2 na 3 usiku na mpenzi wake, wakati huo akiwa mahututi.



Mwenyekiti wa THBUB, Jaji mstaafu Mathew Mwaimu alipoulizwa na Mwananchi jana alithibitisha tume hiyo kufika Himo mkoani Kilimanjaro na mikoa ya Dodoma na Singida.



“Ni kweli timu imefika Kilimanjaro na imehoji watu muhimu na ripoti itatolewa baadaye. Kwa sababu walitoka hapa (Dodoma) wakaenda Singida ndio wakaja Moshi.



“Tunaomba umma uvute subira tukamilishe uchunguzi,”alisema Mwaimu.



Mei 10 mwaka huu, tume hiyo ilitangaza kufanya uchunguzi huru na taarifa zinazokinzana kutoka Jeshi la Polisi, UDOM, Hospitali ya Faraja na za wananchi kupitia mitandao ya kijamii kuhusu kiini cha kifo cha mwanafunzi huyo.



Kwa mujibu wa kifungu cha 15(1) cha sheria ya tume hiyo, sura 391, tume ina mamlaka ya kuanzisha uchunguzi wake juu ya malalamiko yanayoashiria uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji misingi ya utawala pasipo kusubiri.





Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Hospitali ya Faraja, Dk Peter Minja alisema juzi walifika watu kutoka THBUB kujua kama mwanafunzi huyo walimtibia.



"Walikuja hapa hospitalini wakaongea na aliyemhudumia mgonjwa, kikubwa walitaka uthibitisho kujua kama Nusura aliletwa hapa na mwisho wa siku waliondoka," alisema Dk Minja.



Hivi karibuni, dada wa marehemu, Kuruthumu Hassan alieleza kushangazwa mwili wa marehemu Nusura kupelekwa ukiwa umevalishwa kanzu wakati Nusura alikuwa ni mwanamke.



Kuruthumu alisema hadi sasa hawajashirikishwa kuhusu kifo cha ndugu yao huyo na hawajui matapishi na mabaki ya chakula waliyoyaona kwenye moja ya nguo za marehemu, ambayo wanazo taarifa yamepelekwa kwa mkemia.



Awali, mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Amina Shaban, alisema Aprili 29 mwaka huu alimpigia simu mtoto wake, lakini iliita na haikupokewa, kitendo kilichompa hofu kwa kuwa sio kawaida yake.



Alisema ikabidi afanye juhudi kutafuta namba ya simu ya rafiki yake ambaye pia ni mwanafunzi.



Alisema siku iliyofuata alimpigia mwanafunzi huyo aliyemjulisha mtoto wake hayupo chuo alikwenda kwa mchumba wake aliyeko Marangu Kilimanjaro.



 Mwanafunzi huyo alifariki dunia Mei mosi katika Hospitali ya Faraja huku mazingira ya kifo hicho yakizua utata baada ya kuhusishwa na ajali iliyotokea Dodoma, ikimhusisha pia Naibu Waziri wa Tamisemi, Dk Festo Dugange.

0 Comments:

Post a Comment