Mwanza. Baadhi ya wahadhiri na wanazuoni jijini Mwanza wamesema lugha inayotumika kuwapatia ujuzi na maarifa wanafunzi ndiyo chanzo cha wahitimu wa vyuo vikuu na vyakati kukosa ajira.
Wakizungumza kwenye mdahalo wa kutoa maoni juu ya mabadiliko ya sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 uliyofanyika Mei 24, 2023 Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino (Saut) mkoani Mwanza, wamesema sera ya lugha ya kufundishia kuanzia ngazi ya sekondari hadi vyuoni ni sababu wahitimu kushindwa kupata maarifa yatakayowawezesha kupata ajira na kuendana na soko.
“Ninafikiri shida kubwa inayowafanya wahitimu wetu kushindwa kuendana na soko la ajira ni kukosa maarifa ya kutosha na hayo yanasababishwa na lugha inayotumika kuwapatia maarifa hayo kwa maana nyingine hawapati maarifa ya kutosha kutokana na kile wanachotumia kujifunzia,”amesema Getruda Chagaka, Mhadhiri na mbobevu katika masomo ya Lugha ya Kishwahili katika chuo hicho.
Mwanafunzi mwaka wa kwanza Shahada ya Uzamili katika masomo ya Lugha, Savio Francis amesema mbali na lugha ya Kiswahili na kiingereza zote kuwa bora katika kufundishia Serikali inatakiwa kuchagua lugha moja itakayokuwa nzuri zaidi katika kufundishia na wanafunzi kuelewa.
“Mimi kwa upande wangu naona lugha zote ni bora na kama tunahitaji lugha ya Kiswahili itumike katika kufundishia saizi ni mapema sana mazingira yaandaliwe ya kukiboresha, tafiti zifanyike, misamiati iongezwe na pawepo na mazingira mazuri ya kuwaandaa na kuwapata walimu watakaofundisha lugha hiyo,” amesema Francis
Mratibu wa mdahalo huo ambaye pia ni Mhadhiri kutoka Idara ya Elimu Msingi, George Helman amesema mbali na kuwepo kwa mvutano wa lugha sahihi ya kufundishia bado Serikali inapaswa kuangalia upya eneo la masuala mtambuka, falsafa na maadili ili kupata watu sahihi watakao leta maendeleo.
“Masuala mtambuka hayajawekwa vizuri na hivyo yataonekana kwenye mapendekezo ambayo tumeyatoa lakini pia suala la falsafa na maadili limewekwa kwa wepesi sana kwasababu nchi yetu ili kuweza kuhama kutoka hapa tulipo kwenda mbele zaidi tunatakiwa kuanza na maadili ukiangalia nchi zilizoendelea wananchi wake wote wanamaadili,” amesema Helman
0 Comments:
Post a Comment