Sunday, 28 May 2023

Yanga Yawatuliza Mashabiki

TULIENI tunawaua kwao! Hivyo ndivyo walivyoanza kusema Yanga baada ya kumalizika kwa mechi yao dhidi ya USM Alger, ukiwa ni mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambao ulimalizika kwa kufungwa kwa mabao 2-1 kwenye Dimba la Mkapa, Dar jana.

Yanga wametoa kauli hiyo ya kujiamini kutokana na rekodi nzuri waliyonayo ya kushinda mechi zao za ugenini kwenye michuano hiyo kwa msimu huu.

Katika michezo sita ambayo Yanga wameicheza ugenini kwenye kombe hilo katika msimu huu wamefungwa mechi moja pekee, wakiwa na sare moja na wakishinda mechi nne zikiwemo dhidi ya vigogo TP Mazembe, Rivers United na Marumo Gallants.

Yanga walipoteza kwenye mchezo huo licha ya kuwa walionyesha ushindani mkubwa kwa Waarabu hao licha ya mchezo huo kwa kiasi kikubwa kuharibiwa na mvua huku bao lao likifungwa na straika hatari, Fiston Mayele dk 81.

Mabao ya Waarabu yalifungwa na Aymen Mahious dakika ya 32 na Islam Meruli dk 84.

Kwa sasa Yanga wanahitaji ushindi wa mabao 2-0 kwenye mchezo wa marudiano utakaopigwa Juni 3, nchini Algeria kwa ajili ya kubeba ubingwa wa kombe hilo baada ya kichapo hicho.

Kabla ya mchezo huo kulizuka vurugu kubwa ambayo ilisababishwa na mashabiki ambapo kwa mujibu wa taarifa ambayo ilitolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu vurugu hizo zilisababisha kifo cha mtu mmoja sambamba na majeruhi wengine 30 ambao walifikishwa kwenye Hospitali ya Rufaa Temeke.

0 Comments:

Post a Comment