Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wadau wakitaka Serikali ifanye marekebisho ya sheria ya ndoa, Mahakama Kuu ya Tanzania imeipa miezi sita kufanya marekebisho.
Mahakama imetoa muda huo ili Serikali ifute katika vitabu vyake vya sheria, vifungu vya sheria ya ndoa vinavyoruhusu mtoto kuolewa chini ya miaka 18.
Maelekezo hayo ya Mahakama yamo katika hukumu ya kesi namba 14 ya 2022 iliyofunguliwa na Mary Mushi, iliyotolewa Juni 14, 2023 na Jaji Moses Mzuna wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam na nakala kupatikana jana.
Katika hukumu hiyo, Mahakama imemshukia Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro kwa kutoa taarifa kwa umma, akialika maoni ya wadau juu ya umri wa mtoto wa kike kuolewa, wakati tayari kuna uamuzi wa Mahakama.
Itakumbukwa, Oktoba 23, 2019, Mahakama ya Rufani ilitamka kuwa vifungu vya 13 na 17 vya sheria ya Ndoa, sura ya 29 marejeo ya 2002 ni kinyume cha Katiba, hivyo Serikali kupewa mwaka mmoja, kurekebisha vifungu hivyo vya sheria.
Mahakama ilimwelekeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kurekebisha masharti ya kifungu cha 13 na 17 cha Sheria ya Ndoa na badala yake kuweka miaka 18 kama umri unaostahili kuoa na kuolewa kwa wavulana na wasichana.
Hata hivyo, Serikali kupitia kwa Wizara ya Katiba na Sheria ilianza kukusanya maoni ikieleza kuna mkanganyiko wa tafsiri ya kisheria wa umri wa mtoto ulioifanya Mahakama kuielekeza Serikali kufanyia marekebisho sheria hiyo.
Serikali ilisema tangu kutolewa kwa amri hiyo imeendelea na utekelezaji wake, ikiwemo kupeleka muswada bungeni wa marekebisho ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ili kuweka masharti ya kusawazisha umri wa kuoa au kuolewa.
Kulingana na taarifa hiyo, wizara iliwasilisha bungeni mapendekezo ya marekebisho ya sheria ili kusawazisha umri, lakini hata hivyo ikasema ilipendekeza umri wa chini wa kuolewa uwe miaka 15 kwa masharti sita kuzingatiwa.
Masharti hayo ambayo yanapaswa kuzingatiwa ni mtoto husika haangukii kwenye masharti ya Sheria ya Elimu, wazazi wameridhia kwa kiapo kuwa mtoto aolewe, Kamishna wa Ustawi wa Jamii ametoa kibali cha mtoto husika kuolewa.
Pia masharti mengine ni Msajiii wa Vizazi na Vifo amethibitisha umri wa mtoto, daktari amethibitisha kuwa mtoto ana uwezo wa kuingia kwenye ndoa na viongozi wa kidini wameridhia uwepo wa ndoa ya chini ya miaka 18.
Kauli hii ya Waziri ndiyo iliyomsukuma Mary Mushi kufungua kesi hiyo akiiomba mahakama itoe amri kuwa hakuna mkanganyiko wowote kuhusiana na hukumu ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.
Pia, akasema kutokana na uamuzi wa mahakama, ukusanyaji wa maoni unaofanywa na Serikali nchi nzima kwa hisia kuwa kuna mkanganyiko ni potofu, zisizostahili, na zina nia ya kukejeli mamlaka na hadhi ya mahakama ya Tanzania.
Halikadhalika akajenga hoja kuwa vifungu namba 13 na 17 vya sheria ya ndoa vilifutwa moja kwa moja kutoka kwenye kitabu cha sheria kuanzia Juni 7, 2027 ilipotolewa hukumu ya kwanza na kukoma kutumika kisheria.
Mushi, aliyewakilishwa katika kesi hiyo na wakili John Seka, pia alijenga hoja nyingine kuwa kuendelea kuwepo kwa vifungu hivyo katika sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ilikuwa ni kudharau amri ya Mahakama ya Rufani Tanzania.
Katika hukumu yake, Jaji Mzuna alisema mwombaji alikuwa sahihi kupeleka maombi hayo kuomba usikivu wa mahakama juu ya kile alichofanya Waziri wa Katiba na Sheria, hivyo mahakama hiyo ilikuwa na mamlaka kusikiliza kesi hiyo.
Jaji Mzuna alisema upande wa Serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ulishindwa kutekeleza marekebisho ya sheria hiyo kulingana na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa na hakukuwa na mchakato wowote wa kupitia upya uamuzi wao huo.
“Bila kumung’unya maneno ni kwamba waziri anachofanya ni kudharau madaraka iliyokabidhiwa kwa Mahakama hii na Mahakama ya Rufani au Mahakama kuwa zaidi maalumu. Waziri achilia mbali wananchi kwa ujumla, nina wasiwasi, hawezi kukwepa maneno ya wazi ya hukumu mbili zilizotajwa,” alisema.
“Kwa mimi ni wa mtazamo uliowekwa kwamba mashauriano ya umma ni kinyume kabisa na roho ya Katiba ambayo aliteuliwa na kuapa kuitii. Hakuwezi kuwa na marekebisho ya kifungu cha 13 na 17 cha Sheria ya Ndoa tena kwa kisingizio kwamba hailingani na vifungu vingine vya sheria.
“Kwa upande wetu, tayari kuna sheria iliyopingwa ambayo Serikali kupitia maagizo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yanapaswa kutekelezwa na marekebisho hayo yalipaswa kufanyika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja,” alieleza Jaji.
“Wala hakukuwa na maombi ya kuongeza muda. Kushindwa kuzingatia uamuzi huo wa Mahakama, kwa maana ya vifungu vilivyotajwa ambavyo vilitangazwa kuwa kinyume na Katiba, zinakuwa hazifai,” alisema Jaji Mzuna na kuongeza;
“Huo ndio msimamo wa sheria ilivyo. Kwa hivyo, mashauriano yanayoendelea nchini kote ambayo yanalenga kujadili jambo lililokwishahukumiwa na kwa umakini zaidi kwa njia tofauti zaidi au kuifungua tena.
“Mbaya zaidi, baada ya kupita kwa muda fulani, inaonekana kuishushia hadhi mahakama kama mamlaka ya mwisho ya utoaji haki iliyofunikwa vizuri chini ya aya ya 6 ya hati ya kiapo ya mwombaji,” alisisitiza Jaji huyo.
Kuhusu hoja ya kuidharau mahakama, swali linabaki kama taarifa ya umma iliyotolewa na Waziri wa Katiba na Sheria ni sawa na kudharau amri ya Mahakama na Mahakama ya Rufaa katika hukumu ya kesi kati ya AG dhidi ya Rebeca Gyumi.
“Neno kudharau Mahakama kama inavyofafanuliwa katika Shule ya Sheria ya Cornel, Taasisi ya Habari za Kisheria ni kutotii amri ya mahakama,” alisema Jaji Mzuna.
“Zaidi ya hayo, mwenendo unaoelekea kuzuia au kuingilia utaratibu usimamizi wa haki pia ni sawa na kudharau mahakama. Ni sheria ndogo katika nchi yetu dharau inaletwa na mashauri ya dharau ambayo ni kutetea utawala wa sheria.
“Hata hivyo, kama ilivyowasilishwa na Kimario kwa umma notisi ni mchakato wa kutunga sheria ambao Serikali ilipaswa kuufuata kutekeleza agizo la Mahakama”.
Jaji alieleza kuwa Mahakama Kuu ina uwezo wa kudhibiti uamuzi wa chombo cha utawala kwa njia ya mapitio ya Mahakama na kwamba katika hilo la dharau, mwombaji alikosea, kwani ilipaswa kuletwa kama maombi baada ya kupata kibali.
Kulingana na mamlaka iliyopewa kikatiba, Jaji Mzuna alizingatia ukweli kuwa tayari kuna amri ya mahakama juu ya jambo hilo ambayo haijazingatiwa au kuna hatua ikidai kuitii kwa njia tofauti, mahakama inatoa muda wa miezi sita.
“Mwanasheria Mkuu wa Serikali anaelekezwa tena ndani ya miezi sita mingine kuanzia leo kutekeleza maamuzi ya Mahakama ambayo yanapaswa pia kuonyeshwa kwa kufuta na masharti yaliyotangazwa kinyume na katiba katika Sheria ya Ndoa katika Toleo Lililorekebishwa la 2019,” alisisitiza Jaji.
Hata hivyo, juzi Mwananchi ilimtafuta AG Jaji Eliezer Feleshi kuhusu hatua gani itachukuliwa na Serikali lakini hakupatikana. Lakini alipatikana Waziri Ndumbaro ambaye alisema, “Sijapata bado hiyo ruling, nikishaipata nitawasiliana na mwanasheria mkuu wa Serikali ambaye kimsingi yeye ndiye anayeshtakiwa.
“Akishaniambia msimamo wa Serikali katika hilo ndio nitaweza kulizungumzia suala hilo.”
Taarifa hiyo ya umma iliyorejewa na Mahakama ni ya Septemba 28, 2022 ambayo ilisainiwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro ikielezea shughuli ya kukusanya na kuchambua maoni ya maboresho ya Sheria ya Ndoa ili kutatua changamoto ya kukosekana kwa tafsiri moja ya kisheria ya umri wa mtoto kuoa na kuolewa.
Katika taarifa hiyo, ilisema baada ya shughuli hiyo kukamilika Serikali itawasilisha bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na hatimaye kupitishwa.
“Kwa sasa wizara inaendelea na ukusanyaji wa maoni ambapo imeendelea kukutana na wadau na makundi mbalimbali, wakiwemo Kamati za kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, wabunge, viongozi wa dini, viongozi wa kimila, waendesha bodaboda,” alisema.
Machi 22, 2023 Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) lililokoleza moto wa umri halali wa mtoto wa kike kuolewa, pale lilipopendekeza mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 11, 12 ambaye hajaendelea na masomo aweze kuolewa.
Akitoa maoni mbele ya Tume ya Haki Jinai, mwanasheria wa baraza hilo, Hassan Fatiu alipendekeza mtoto mwenye umri wa miaka 11, 12 au 13 aliye balehe aruhusiwe kuoa kwa uhalali wa mahakama utakaozingatia vielezo vya kimazingira.
“Mtoto wa kike ana miaka 11, 12 hajaendelea na elimu, kwanini asiolewe? Ukimuacha huyu ni matokeo ya kupata mimba mtaani. Simaanishi kila mtoto wa umri huo aruhusiwe kuolewa, ila mahakama itajiridhisha,” alisema Fatiu.
“Sisi tumependekeza sheria ibakie kama ilivyo na hatulazimishi kila mwenye umri huo aolewe. Kwa yule atakayeoa umri uo kabla mahakama kuthibitisha basi ahesabike kutenda kosa,” alisema mwanasheria huyo akitoa mapendekezo hayo.
Hata hivyo, mapendekezo hayo hayakuwafurahisha wanaharakati, hususan Rebecca Gyumi wa Shirika la Msichana Initiative, ambaye ni mmoja wa wanaharakati aliyefungua kesi ya kupinga suala hilo na kushinda.
Mwanaharakati Ananilea Nkya alisema hatua ya Serikali kuanza kukusanya maoni ni kudharau uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Rufaa kwa sababu tayari ilishatoa maelekezo kuwa ndani ya mwaka mmoja vifungu hivyo viwe vimebadilishwa.
“Kama mihimili haiingiliani basi Serikali inapaswa kujitathmini na kueleza inafanya kazi kwa ajili ya nani maana mahaka ilitoa uamuzi kwa manufaa ya wananchi, yenyewe ikashindwa kutekeleza. Hii nchi ni ya kidemokrasia, ni lazima Serikali ifanye kazi kwa ajili ya wananchi, sasa ituambie vikwazo nini kubadilisha hivyo vifungu.”
Ananilea ameyataka mashirika na asasi za kiraia zinazohusika na utetezi wa wanawake na watoto kuimarisha ufuatiliaji wa uamuzi huo mpya wa mahakama na kuisukuma Serikali kuhakikisha inarekebisha vifungu hivyo katika muda ulioelekezwa na mahakama.
Nyongeza na Elizabeth Edward
0 Comments:
Post a Comment