Friday 23 June 2023

Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalumu Kupata Vifaa Vya Kisasa

Dar es Salaam. Jumla ya wanafunzi 100 wa shule za msingi na sekondari wenye ulemavu wa macho katika mikoa sita, wana kila sababu ya kutabasamu baada ya Kilimanjaro Blind Trust Africa (KBTA) kutoa msaada wa vifaa vya Orbit Readers 20 vyenye thamani ya Sh192 milioni.

Vifaa hivyo, vitawawezesha katika mchakato wa kujifunza pamoja na kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ya kidijitali, vinakwenda Shule ya Msingi Ilembula (Iringa), pamoja na Shule ya Msingi Malangali (Morogoro).

Shule zingine ambazo zitanufaika na msaada huo ni Sekondari ya Wasichana Korogwe (Tanga), Sekondari ya Mkolani (Mwanza), Sekondari ya Mtera (Dodoma) na Sekondari ya Kantalamba (Rukwa).

Orbit Reader 20 ni kifaa cha kipekee ambacho kinafanya kazi tatu ambapo kitamwezesha mtumiaji kisoma vitabu, kuandika na kuchukua madokezo, na kwamba kinaweza kuunganisha kwenye kompyuta au simu janja kupitia USB au Bluetooth.

 “Vifaa hivi ni vya kisasa na vinakwenda pamoja na ulimwengu wa teknolojia ya kidijitali itasaidia wanafunzi hawa wasiachwe nyuma katika teknolojia, hivyo natoa wito kwa walimu kuhakikisha watumiaji wanavitunza kwa manufaa yao wenyewe,” alisema Afisa Mtendaji Mkuu wa KBTA Suparna Biswas.

Amesema lengo la shirika hilo ni kuhakikisha wanafunzi wenye changamoto ya kutoona wanapatiwa vifaa hivyo ili waweze kuendana na teknolojia ya sasa badala ya kubaki nyuma, na akatoa wito kwa serikali na wadau mbalimbali sekta binafsi kusaidia upatikanaji wa vifaa hivyo kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kutoona.

Tangu mradi huo uanzishwe nchini mwaka 2021 jumla ya vifaa 317 vyenye thamani ya Sh600.8 milioni tayari vimesambazwa katika shule 20 za msingi na sekondari katika mikoa mbalimbali.

Wakati huo huo, Katibu wa Taifa wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata) Jonas Lubago amesema kuwa idadi ya watoto wasioona shuleni ni kubwa hivyo wadau mbalimbali waendelee kuwasaidia kwani miongoni mwa changamoto zinazowafanya washindwe kuendelea na masomo ni pamoja na kutopatikana kwa vifaa maalum kwa ajili yao.

 “Kwa sasa kuna wanafunzi wasioona zaidi ya 1000, hivyo mahitaji bado ni makubwa ili waweze kwenda na ulimwengu wa kidijitali, tunashukuru shirika hili kwa mchango wao unaolenga kulea watoto wenye ulemavu wa aina hiyo,” alisema.


0 Comments:

Post a Comment