Saturday 29 July 2023

Benki Zatakiwa Kupunguza Riba Ili Kutoa Fursa Kukopa

BENKI na taasisi mbalimbali za fedha nchini zimetakiwa kupunguza riba na gharama za mikopo, ili kutoa fursa kwa wanawake wajasiriamali kukopa na kufanya uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo katika Jukwaa la Utayari na fursa lililoandaliwa na Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kupitia mradi wake wa Employment and Skills for the Development in Afrika (E4D).

Amesema ni muhimu benki nchini kuwa na mikopo rafiki riba nafuu kwa wanawake kwa sababu ndio watu wenye uhakika wa kurejersha fedha hizo kuliko wanaume ambao mara nyingi wamekuwa ni shida.

“Niwasihi benki mbalimbali kupunguza riba ili iweze kuendana na kasi ya kina mama wanayokwenda nayo, kutokana na riba kuwa juu ndio maana wanawake wanapata shida na kukimbilia mikopo ya halmashauri ya asilimia 10 ambayo peke yake haiwezi kuwatosha,” amesema

Aidha amesema kuwa zipo changamoto mbalimbali ambazo wanawake wanazipitia katika masuala ya fursa, mitaji na masoko ambazo zinapaswa kutatuliwa ili kuliwezesha kundi hilo kufanya biashara kwa uhuru na kujiingizia kipato.

“Moja ya suluhisho la jambo hilo ni kutumia masoko mtandao, hii ni fursa ambayo ikitumiwa vizuri itawakomboa wanawake wengi kiuchumi, leo hii mjasiriamali unayefikiria kutengeneza batiki na umepanga kutumia milioni 10 tenga kiasi kingine kwa ajili ya soko mtandao ambalo ukilitumia vizuri itakusaidia kujitangaza na kuuza bidhaa zako,” amesema

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TWCC, Mercy Sila amewataka wanawake kuungana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuweza kuingia katika masoko makubwa ya kimataifa ya biashara na hatimaye kujikwamua kiuchumi.

Sila amesema kwa sasa fursa za kiuchumi ni nyingi na Serikali imekwisha weka mazingira wezeshi ya wanawake kujikwamua hivyo ni muhimu kwa kundi hilo kuungana kwa pamoja na kufanyakazi kwa ushirikiano.

“Tukiungana tutafanikiwa kwa haraka, kama kuna mtu amepata oda kubwa ya bidhaa mbalimbali ni muhimu kuungana na mwenzake kuweza kufanikisha hilo, tunayasema haya kwa sababu tunataka wanawake kutoka chini nao waweza kunyanyuka kwa pamoja na wenzao waliofanikiwa,” amesema

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Mwajuma Hamza amesema kazi yao ni kuhakikisha kwamba wanawake wanapata fursa za kiuchumi, wanashiriki kuzalisha ajira, kukuza kipato na kuchangia pato la taifa.

“Ili kuendana na mabadiliko la tekonolojia tumezindua pia soko mtandao kwa ajili ya wanawake ambapo wataweza kutumia simu janja yake na kuingia google na kupakua app ambayo imeandikwa iSoko, ukajisajili na kuweka bidhaa zake huko na mtu yoyote aliyopo nchini na nchi zingine za Afrika ataona,” amesema

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ-E4D), Kabongo Mbuyi amesema wameamua kufadhili jukwaa hilo na kushirikiana na TWCC kwa lengo la kuwawezesha wanawake wajasiriamali kujikwamua kiuchumi.

“Tumekuwa tukifadhili program mbalimbali za wanawake lakini tumevutiwa na TWCC kwa kuwa wanafanya kazi kubwa ya kuwainua wanawake lengo likiwa wajikwamue kichumi na kukuza pato la taifa la Tanzania,” amesema

0 Comments:

Post a Comment