Thursday 6 July 2023

Sera Mpya Ya Elimu Itamtaka Mwanafunzi Kuwa Shuleni Miaka Kumi Tu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof.Adolph Mkenda amesema mageuzi yajayo ya Sera ya Elimu nchini yatakayojikita kumuongezea ujuzi zaidi kijana akiwa shuleni yatachangia vijana wengi kujiajiri kulingana na mazingira yanayomzunguka. Waziri Mkenda amesema hayo wakati wa majumuisho ya ziara yake ya siku moja Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza baada ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara yake vikiwemo vyuo vya ufundi Veta,amebainisha mafunzo ya Amali kama yanavyojulikana yataanza muda siyo mrefu mara baada ya Sera hiyo kupita kwenye hatua za mwisho mwisho. “Sera hiyo mpya itamtaka mwanafunzi kuwa shuleni kwa miaka kumi tu atasoma hadi darasa la sita akifaulu atalazimika kuingia kidato cha kwanza hadi cha nne huko sasa atakutana na mafunzo kwa vitendo zaidi na akihitimu anatoka na ujuzi husika utakaokuwa mkombozi katika shughuli aliyolenga”, amefafanua Prof Mkenda.

Aidha Prof Mkenda ameongeza kuwa Mkoa kama wa Mwanza mafunzo hayo ya Amali yatawanuisha wale watakaojikita kwenye Uvuvi kwani wakihitimu watakuwa na ujuzi wa kutosha kwenye sekta hiyo tofauti na ilivyo sasa.

Waziri Mkenda amebainisha utekelezaji huo ni ahadi ya Rais Dkt.Samia Suluhu aliyoitoa Bungeni ya kuleta mageuzi kwenye sekta ya elimu kwa kutaka yawepo mafunzo zaidi ya kuwaongezea ujuzi ili kuweza kuzimudu fursa mbalimbali zilizowazunguka.

Huu mchakato wa sera mpya ya elimu umeanza siku nyingi kwa kuwashirikisha wataalam na wadau,nawathibitishia sasa upo ukingoni kusubiri hatua kadhaa za mwisho mwisho za kupitiwa na Makatibu wakuu na Baraza la Mawaziri kabla ya kumfikishia rasmi Rais ili kumuomba aridhie,

“Prof.MkendaAkiwa kijiji cha Karumo Wilayani Sengerema ameshuhudia maandalizi ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi Kampasi ya Mwanza kitakacho kamilika Octoba mwakani kilichoghalimu zaidi ya Shs bilioni 18.

“Mhe Waziri Chuo hiki kitachukua muda wa miezi 15 kukamilika na kuanza kutoa mafunzo,wiki chache zijazo tunatarajia kumpata Mkandarasi,hapa kutakuwa na kozi 35 zikiwemo za kuwapata Wataalamu wa kupima ardhi kupitia majini, watatuzi wa migogoro ya ardhi na mafunzo ya amali pia yatatolewa hapa chuoni,”Prof.Evaristo Liwa,Makamu Mkuu Chuo Kikuu Ardhi.

Aidha Waziri Mkenda ameshauri mara baada ya Chuo hicho kukamilika kuwepo na mpango wa kuwapata baadhi ya wahadhili kutoka nje ya nchi watakaongeza utoaji wa elimu bora na kubadilishana uzoefu na watalaam wa hapa nyumbani. Waziri huyo wa Elimu,Sayansi na Teknolojia akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Seni Ngaga amefika Halmashauri ya Buchosa na kushuhudia maandalizi ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Veta kitakachoghalimu Shs bilioni 3 Pia akiwa mjini Sengerema amekubali kukipokea Chuo cha Ufundi Veta mara baada ya uongozi kuwasilisha barua rasmi ya ombi hilo, awali Chuo hicho kilikuwa kinamilikiwa na Halmashauri ya Sengerema.

 

0 Comments:

Post a Comment