Tuesday, 25 July 2023

Wanawake Waamriwa Kufunga Biashara Za Saluni

Maelfu ya maduka hayo ya urembo yanatarajiwa kuwa yamefunga milango yake leo hii Jumanne kulingana na amri iliyotolewa mwezi uliopita na utawala wa Taliban.

Wizara ya Kuendeleza Maadili na Kinga dhidi ya Tabia Potofu ilitoa muda wa kufungwa saluni zote hadi kufikia leo hii Jumanne, ikisema kuwa kipindi hicho kilikusudiwa kuwaruhusu wanawake kumalizia shughuli na bidhaa zao za urembo walizolimbikiza hadi kufunga maduka yao.

Mwanamke anayeendesha biashara ya saluni akifunga virago vyake kutii amri ya serikali ya Taliban.Picha: ALI KHARA/REUTERS
Wizara hiyo ya kuendeleza maadili imesema vipodozi vingi vinawazuia wanawake kutawadha au kushika udhu kwa ajili ya sala ikiwa ni pamoja na urembo wa kuongeza kope na kusuka nywele ambao pia umepigwa marufuku.

Utawala wa Taliban umesema sababu kubwa ya kuchukua hatua hiyo ni kutokana na kwamba fedha nyingi zinatumika katika anasa za urembo na kusababisha hali ngumu hasa katika familia maskini na kubwa zaidi virembesho hivyo na huduma za urembo kwa jumla hazizingatii maadili ya dini ya Kiislamu.

Soma:Kiongozi wa Afghanistan asema hadhi ya wanawake imebadilika

Mama mmoja ambaye anaendesha biashara ya saluni amesema Wataliban wanapaswa kufikiria upya juu ya amri yao hiyo kwa kuzingatia miaka mingi ya kazi ngumu na uwekezaji mkubwa katika kujenga biashara za wanawake.

Tangu ilipoingia madarakani mnamo mwezi Agosti mwaka 2021, serikali ya Taliban imepitisha amri ya kuwazuia wasichana kuhudhuria masomo kwenye shule za upili na kwenye vyuo vikuu, vilevile wanawake nchini humo wamepigwa marufuku kujipumzisha katika sehemu za mabustani, na kushiriki michezo kwenye viwanja vya michezo na kumbi za mazoezi, na vilevile wameamriwa kujifunika wanapokuwa hadharani.

Maelfu ya wafanyikazi wa serikali wanawake walipoteza kazi zao mara Taliban ilipochukua madaraka na serikali hiyo kuamua kuwalipa ili wasalie nyumbani.

Waziri Mkuu wa Afghanistan chini ya utawala wa Taliban Molawi Abdelkabir.
Waziri Mkuu wa Afghanistan chini ya utawala wa Taliban Molawi Abdelkabir.Picha: mehrnews
Chama cha Wafanyabiashara na Viwanda cha Wanawake wa Afghanistan kimesema marufuku hiyo kwa wanawake wanaoendesha maduka ya urembo itasababisha takriban wanawake 60,000 wapoteze mapato kutokana na kuacha kazi katika saluni zipatazo 12,000.

Soma:Vizuizi dhidi ya wanawake ni uhalifu dhidi ya ubinaadamu

Richard Bennett, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan kwenye ripoti yake kwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi uliopita, alisema wanawake na wasichana wa Afghanistan ni miongoni mwa watu wanaokabiliwa na masaibu mabaya zaidi duniani.


0 Comments:

Post a Comment