Thursday, 5 October 2023

Waziri Mkuu Ameagiza Watumishi Kusimamishwa Kazi

 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Elikana Balandya kuwasimamisha kazi watumishi wa idara za mipango miji na ardhi wa jiji la Mwanza.



Waliogizwa kusimamishwa kazi ni pamoja na mkuu wa idara ya mipango miji, Robert Phares na ofisa mteule na mkuu wa kitengo cha Ardhi katika Jiji la Mwanza, Halima Iddi Nasoro



Mbali na hilo na Majaliwa ameagiza Kaimu Kamishna wa Ardhi Msaidizi (Mwanza) Elia Kamihanda kurudishwa makao makuu ili kuchukuliwe hatua za kinidhamu



Majaliwa ametoa maagizo hayo jana Jumanne Oktoba 3,2023 kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma cha viongozi wa majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga na Dodoma ili kujadili migogoro ya ardhi iliyokithiri kwenye majiji hayo.



Ingawa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa vyombo vya habari haikufafanua kwa kina sababu za hatua iliyochukuliwa na Majaliwa dhidi ya watumishi hao, lakini Jiji la Mwanza limekuwa na changamoto kuuza viwanja kinyume cha utaratibu.



Januari 13, 2023, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima 'alimshitakii' aliyekuwa mkurugenzi jiji hilo, Sekiete Seleman kwa Tamisemi akimtuhumu kuuza viwanja viwili vyenye thamani ya Sh1bilioni.



Pia Malima aliagiza watumishi wanne wa jiji hilo kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi kwa tuhuma za uuzaji wa viwanja hivyo.Waliosimamishwa ni mhasibu wa jiji, mwanasheria, ofisa manunuzi na ofisa mipango.



Watumishi hao wa umma wanadaiwa kuuza viwanja hivyo vilivyopo mtaa wa kibiashara katikati ya jiji kwa thamani ndogo kulinganisha na bei ya soko. Wanadaiwa kuviuza viwanja bila kufuata utaratibu.



Katika kikao chake cha leo Majaliwa alisema, “naagiza Katibu Tawala wa Mkoa wasimamishe kazi mkuu wa idara ya mipango jiji, ofisa mteule na mkuu wa kitengo cha ardhi katika jiji la Mwanza.



“Pia kaimu kamishna wa ardhi msaidizi, arudishwe makao makuu na kuchukuliwa hatua za kinidhamu.’’ amesema Majaliwa.



Katika hatua nyingine, Majaliwa ameagiza ujenzi wa ghorofa uliositishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla uendelee kwenye viwanja namba 194 & 195 kitalu ‘U’ Rwagasore, katika jiji la Mwanza na wamiliki wa viwanja hivyo wakabidhiwe hati zao.



Katika hatua nyingine, Majaliwa ameliagiza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwafuatilia na kuwarejesha Dodoma watumishi 11 waliokuwa halmashauri ya jiji la Dodoma ili wajibu tuhuma za matumizi mabaya ya fedha, kupora maeneo ya wananchi na kugawa maeneo ya wazi.



Amewataja watumishi hao kuwa ni Josephat Mafuru (aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji), Scorpion Philip, Lennis Ngole, Allen Mwakanjuki, Aisha Masanja, Agusta Primo, Azory William Byakanwa, Frezia Kazimoto, Premin Nzenga, Stella Komba na Thabiti Mbiyagi.

0 Comments:

Post a Comment