Dar es Salaam. Baada ya kuwapo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu gharama za vifurushi vya bima za afya, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema bei zimepunguzwa.
Na sasa mtu anaweza kupata kifurushi cha Sh168,000 kwa mwaka sambamba na uwepo wa vifurushi mbalimbali ikiwemo vya watoto.
Hili linasemwa wakati ambao tayari utekelezaji wa sheria ya bima ya afya kwa wote umeanza, huku utaratibu maalumu ukiwa umewekwa ili kuwafikia wale wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama ikiwemo kaya maskini.
Hayo yamesemwa na Meneja wa NHIF ofisi ya Temeke, Cannon Luvinga wakati akizungumza na waandishi katika maonyesho ya 49 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF).
Amesema kupungua kwa bei hiyo kunalenga kuwafanya watu wengi zaidi kumudu gharama za matibabu ili kufanikisha utekelezaji wa bima ya afya kwa wote.
“Awali watu waliona bei za vifurushi si rafiki, lakini tulikaa chini tukaweka bei rafiki na sasa Watanzania wanachangamka katika kujiunga ili wawe na uhakika wa matibabu kwani tumesajili vituo zaidi ya 19,000, hivyo Mtanzania aliyejiunga na NHIF hatembei umbali mrefu kufuata huduma,” amesema.
Amesema kwenye Sh168,000 mtu anaweza kupata huduma kwa mwaka mzima huku akisema fedha hiyo ni ndogo na mtu anaweza kulipia kila mwezi.
“Bei zipo mbalimbali kulingana na ukubwa wa familia, umri na tunampa nafasi Mtanzania kuunganisha familia yake,” amesema.
Akizungumzia uwepo wao katika maonyesho hayo amesema mbali na kusikiliza changamoto mbalimbali za wateja pia watakuwa wakisajili wanachama wapya ambao wanatakiwa kuja na namba za Kitambulisho cha Taifa pekee, ili waunganishwe.
“Kwa upande wa watoto mzazi anapaswa kuja na cheti chake cha kuzaliwa ili aweze kuunganishwa. Pia upo utaratibu wa watu wanaotoka kaya maskini kupata huduma hii kupitia Tasaf (Mfuko wa Maendeleo ya Jamii) amesema.
Hili linasemwa wakati ambao Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk Irene Isaka aliliambia Mwananchi kuwa bima ya afya kwa wote inakuja na mfumo utakaomwezesha Mtanzania kujisajili na kulipa kidogokidogo kupitia mawakala, benki na kampuni za simu kuanzia kiasi cha Sh14,000.
Hilo linaenda sambamba na kuweka utaratibu maalumu kwa ajili ya kaya maskini ili kuwaingiza katika mfumo wa bima.
“Lakini pia kuna kifurushi cha bima kwa wote kwa kaya maskini, chenye huduma 277, ambacho kitaanza kutumika kwa gharama ya Sh150,000 kwa kaya ya watu sita, sawa na Sh25,000 kwa kila mtu kwa mwaka. Hii ni gharama nafuu ukilinganisha na gharama halisi ya bima,” amesisitiza Dk Isaka alipofanya mahojiano na Mwananchi.
Kutokana na kushushwa kwa bei za vifurushi, Serikali katika mwaka 2025/2026 ilipendekeza kuanzisha vyanzo vya mapato vinane kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na kugharimia bima ya afya kwa wote.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh586.4 bilioni.
Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alitoa pendekezo hilo alipowasilisha bungeni, mapendekezo ya bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2025/2026.
Alisema hatua hiyo inatokana na mabadiliko ya kisera yanayoendelea duniani ambayo yamesababisha wadau muhimu wa maendeleo kupunguza misaada iliyokuwa inatolewa kwa ajili ya huduma za afya, ikiwamo kukabiliana na kudhibiti magonjwa mbalimbali hususan Ukimwi.
Dk Mwigulu alisema Serikali inapendekeza kuanzisha vyanzo mbadala vya mapato ili kupunguza nakisi ya kibajeti iliyotokana na kupungua kwa misaada kwa kufanya marekebisho katika sheria mbalimbali.
“Inapendekezwa asilimia 70 ya mapato yatakayoongezeka ipelekwe kwenye Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) na asilimia 30 ipelekwe kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote.”
Alisema Serikali inapendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 ili kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vya kilevi vinavyozalishwa na vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi.
Waziri alisema Sh20 kwa lita kwa bia zinazotambulika kwa heading 22.03, Sh30 kwa lita kwa mvinyo unaotambulika kwa heading 22.04, 22.05, na 22.06. Vilevile Sh50 kwa lita kwa pombe kali na vinywaji vingine vinavyotambulika kwa heading 22.08.
Eneo lingine alisema ni kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 ili kuongeza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwenye huduma za mawasiliano ya kielektroniki kutoka asilimia 17 hadi asilimia 17.5.
“Kufanya marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, Sura 220 ili kutoza kiasi cha Sh10 kwa kila lita ya mafuta ya petroli, dizeli na ya taa. Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Madini, Sura 123 ili kutoza kiwango cha asilimia 0.1 kwenye thamani ya soko ya madini,” alisema.
Dk Mwigulu alitaja eneo jingine la chanzo cha fedha ni kufanya marekebisho kwenye Sheria ya
Michezo ya Kubahatisha, Sura 41 ili kuongeza kiwango cha kodi kwenye zawadi ya ushindi kwenye michezo ya kubashiri matokeo kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15 na kwenye michezo ya kasino ya ardhini kutoka asilimia 12 hadi asilimia 15.
Pia kutoza magari na mashine zinazoingizwa kutoka nje ya nchi kwa Sh50,000 kwa magari yenye ukubwa wa injini (CC) kati ya 0 -1000, Sh100,000 kwa magari yenye ukubwa wa injini kuanzia 1001-1500, Sh150,000 kwa magari yenye ukubwa wa injini kuanzia 1501-2500, Sh200,000 kwa magari yenye ukubwa wa injini kuanzia 2501 na zaidi.
Alisema Sh250,000 kwa mashine (excavators, bulldozers, fork lifts) zenye heading 84.29 na 84.27.
“Pia kutoza Sh500 kwa kila tiketi inayotolewa na mtoa huduma za usafirishaji kwa njia ya treni na kutoza Sh1,000 kwa kila tiketi inayotolewa na mtoa huduma za usafirishaji kwa njia ya anga,” alisema.
Akizungumza mmoja wa watembeleaji wa maonyesho hayo, Juma Mussa alitaka gharama za vifurushi kuwekwa wazi ili watu waweze kujua vipi wanavyoweza kumudu.
“Hata mimi ndiyo nasikia kuwa vifurushi vimeshuka bei na mtu anaweza kulipa kidogokidogo, waseme wapi tunaweza kupata hizo bei zote ili tujipime tunachoweza,” alisema Mussa.
0 Comments:
Post a Comment