Sunday, 29 June 2025

Hekaheka Waumini Wa Askofu Gwajima Na Polisi

Dar es Salaam. Ni kama kila mmoja kati ya Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima walikuwa wakisubiri nani aanze.


Ndivyo ilivyokuwa leo Jumapili Juni 29, 2025 waumini wa kanisa hilo walipobadili mbinu ya kufanya ibada barabarani kisha kuibukia kwenye Kanisa la Kiluthel Afrika Mashariki (KKAM) na kufanya ibada kabla ya kutawanywa kwa mabomu ya machozi.

Vuta nikuvute ya polisi na waumini hao ilichukua takribani saa moja hadi eneo hilo kutulia na shughuli nyingine kuendelea.

Hata hivyo, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema: “Tumewakamata 33 na tunawahoji ili kujua wanakitu gani kwa sababu kwenye hilo kanisa wamesali vizuri na sisi tunajua haki za kuabudu na ndio maana hatukuwafanya chochote.”

Amesema wanachoshangaa kama wamemaliza kusali vizuri, “inakuwaje wanatoka na mabango? Ama na hilo kanisa limeanza kuingia barabarani? Sasa ndio tunaendelea kuwahoji na hatujajua kama ni waumini wa Gwajima ama siyo kwa sababu wametoka mule  (kwenye kanisa la KKAM).”

Awali, waumini wa kanisa hilo ndiyo waliamua kuanza kwa kuingia barabarani na mabango, kabla ya Jeshi la Polisi kuwazuia na kuwatawanya kwa kupiga mabomu ya machozi  katika hekaheka hiyo iliyoanza saa 5:42 asubuhi hadi saa 6:45 mchana.

Tukio hilo lilitanguliwa kwa waumini hao kubadili mbinu ya kufanya ibada ya Jumapili barabarani eneo la katikati ya Ubungo Maji na Kibo, jirani na yalipo makao makuu ya kanisa hilo.

Utaratibu wa kusali barabarani wamekuwa wakiufanya tangu Juni 3, 2025 kanisa hilo lilipotangazwa kufutwa na Serikali na mara zote kutawanya na jeshi la polisi.

Kanisa hilo lilifutwa na Juni 3, 2025 na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa kutokana na kile kilichoelezwa kukiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337 kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.

Tayari kanisa hilo, limefungua kesi Mahakama Kuu, Maslaja ya Dodoma kupinga uamuzi huo. Hata hivyo, licha ya kufungua kesi waumini wake wanaendelea kwenda maeneo hayo kila Jumapili.

Kwa wiki mbili mfululizo za kila Jumapili, waumini wa kanisa hilo, wamekuwa wakifika maeneo ya kanisa hilo wakijikusanya na kuendesha maombi huku polisi ikiwa inaendelea kuimarisha ulinzi katika kanisa hilo ambalo limezungushiwa utepe kuzuia mtu yeyote kuingia.

Leo, polisi imedhibiti maeneo yote ambayo waumini hao hujikusanya na kuimarisha doria kuanzia Ubungo Maji hadi Corner, jambo lililosababisha waumini hao kuuangana na wale wa KKAM lililo jirani na kanisa lao kuendelea na ibada.

Wakati ibada hiyo ya Jumapili ya leo Juni 29, 2025 ikiendelea kanisani hapo, askari zaidi ya 20 wakiwa kwenye magari manne walisogea hadi upande wa pili wa barabara takribani umbali wa mita 200 kutoka lilipo kanisa la KKAM wakiwa tayari kwa lolote.

Ilipofika saa 5:42 asubuhi gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeusi ya jeshi hilo ilisogea kama mita 10 kutoka kwenye kanisa bila askari wake kushuka, huku waumini wakiendelea na maombi na mara kadhaa wakinong’onezana kwamba wajiandae kwa lolote.

Mwananchi iliyokuwa eneo la tukio, ilishuhudia waumini hao baada ya ibada wakihamasishana kusogea jirani na barabara ya mchepuko kuonesha mabango waliyokuwa yamebeba yaliyoandikwa kwa maandishi mekundu, huku kwa pamoja wakikubaliana kutorudi nyuma.

Polisi waliokuwa kwenye Toyota Land Cruiser walishuka na kuwazuia kusogea kwenye barabara ya mchepuko, bila mafanikio kabla ya wenzao waliokuwa upande wa pili wa barabara kusogea na kuanza kupiga mabomu ya machozi, jambo lililosababisha taharuki kwa wapita njia na kwa dakika kadhaa kusababisha msongamano kwa magari mengine yaliyokuwa yakipita eneo hilo.

Wakati hayo yakiendelea, polisi iliwakamata watu wawili, kitendo ambacho hakikuwarudisha nyuma wengine ambao waliendelea kupaza sauti wakitaka uhuru wao wa kuabudu uheshimiwe huku mara zote wakihamasishana kutorudi nyuma licha ya polisi kuzidi kupiga mabomu ya machozi.

Hata hivyo, waumini hao walizidiwa nguvu na jeshi la polisi na kuwakamata baadhi yao, huku wengine wakipanda wenyewe kwenye gari za polisi na wale waliokuwa wabishi waliambulia kipigo kutoka kwa polisi na kupandishwa kwa lazima.

Hadi saa 6:45 mchana eneo lote la Kanisa la KKAM lilikuwa limesalia tupu, huku polisi wenye mbwa wakiendelea kuimarisha ulinzi hadi saa 7:30 mchana walipoondoka eneo hilo na kuendelea na doria upande wa Kanisa la Ufufuo na Uzima ambako wamekuwa wakililinda tangu alfajiri ya kuamkia Juni 3, 2025

0 Comments:

Post a Comment