Dar es Salaam. Kila mwaka wa masomo, maelfu ya watoto huacha shule kabla ya kumaliza elimu ya msingi au sekondari.
Tatizo hili ni kubwa kwa mikoa 10 ambako, kwa mujibu wa uchambuzi wa gazeti hili ukitumia takwimu za Serikali, kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaoacha shule katika ngazi ya msingi na sekondari.
Wadau wanasema hali hiyo inasababishwa na changamoto mbalimbali, zikiwamo umaskini wa familia, mimba za utotoni, majukumu ya nyumbani na kukosekana kwa msukumo wa kimasomo kwa baadhi ya wanafunzi.
Takwimu za Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), zinaonyesha mikoa inayoongoza kwa wanafunzi kuacha shule za msingi, ndio hiyohiyo inayoongoza pia kwa shule za secondari.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, wanafunzi 158,374 waliacha shule za msingi na wengine 148,337 wakiacha sekondari mwaka 2023.
Mikoa iliyoongoza wanafunzi kuacha shule za msingi kwa mpangilio ni Tabora, Geita, Kagera, Mwanza, Dodoma, Simiyu, Rukwa, Shinyanga, Kigoma na Singida ikijumuisha karibu ya robo tatu ya wanafunzi wote walioacha shule katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Mkoa wa Tabora uliongoza kwa wanafunzi 21,539 kuacha shule na Geita wanafunzi 20,115. Takribani wanafunzi 6,500 waliacha shule katika mwaka huo kwa kila mkoa.
Wavulana wanaongoza kwa kuacha shule za msingi. Katika kila 10 walioacha shule wavualana walikua takribani sita.
Kwa shule za sekondari mikoa hiyo hiyo ilijirudia, huku mingine mitatu ikitoka na mikoa ya Tanga, Mtwara na Mara kuingia katika mikoa 10 iliyoongoza.
Katika mikoa 26 zaidi ya nusu ya wanafunzi yaani asilimia 55 walitoka kwenye mikoa 10. Kwenye kila mkoa angalau wanafunzi 5,900 waliacha shule. Geita ikiongoza kwa wanafunzi 11,146.
Kwa sura ya kijinsi wavualana ndio walioongoza kuacha shule za sekondari, kwani katika kila wanafunzi 100 walioacha shule walikuwa wawili zaidi ya wasichana.
Ukatishaji masomo kwa wanafunzi si tu unadhoofisha maisha ya baadaye ya watoto hawa, bali pia unaleta athari kwa maendeleo ya Taifa zima.
Aidha, hali hii inakwamisha juhudi za Serikali na wadau wengine kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan lengo la kuhakikisha elimu bora, jumuishi na yenye usawa kwa wote ifikapo mwaka 2030.
Akizungumzia suala hili, mdau wa elimu na aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa shirika la Uwezo Tanzania, Zaida Mgallah anasema tatizo la watoto kuacha shule huchangiwa na vitu vingi na tatizo huwa kubwa zaidi kwa mikoa ya pembezoni tofauti na ile ya mijini.
Miongoni mwa sababu zinazochangia mikoa hiyo kuongoza kwa idadi kubwa ya wanafunzi wanaoacha shule, anasema ni mazingira ya ujifunzaji shuleni.
Mazingira hayo yanaweza kusababishwa na umbali wanaotembea wanafunzi ili kuifikia shule, hali inayoweza kuwaktisha tamaa kwenda shule.
“Kuna wengine ni watoto wadogo wazazi wanaogopa kuwaacha waende shule kwa kutembea umbali mrefu, huenda kuna pori kuna baadhi ya maeneo pia wazazi wanaogopa sababu ya mwingiliano wa wanyama na binadamu, imefanya pia baadhi ya wazazi kukataza watoto wao kwenda shule. Serikali ijenge shule karibu na maeneo ya wananchi” anasema.
Anasema, njaa ni jambo lingine linalofanya wanafunzi kushindwa kwenda shuleni, hasa ikiwa huduma za chakula hazitolewi.
Anasema kuna wakati Uwezo Tanzania ilifanya tathmini kuangalia utoaji wa chakula kwa watoto walio shuleni sambamba na kuangalia idadi ya wanafunzi wanaokula kabla ya kufika shuleni.
“Ilibainika ni asilimia 39 ya kaya ndiyo walikuwa wanawapa watoto chakula asubuhi na asilimia inayobaki wanaondoka nyumbani hawajala. Kwa upande wa shule za msingi walikuwa asilimia 23 pekee kwa mikoa ambayo ilifanyiwa tafiti. Sasa watoto wengine wanashindwa kushinda na njaa kwa sababu nyumbani hawajala na shuleni hawajala, jambo linalofanya wawe watoro kwa kusikia njaa,” anaeleza.
Matokeo ya kujifunza ni sababu nyingine ya watoto kuacha shule kwani anasema baadhi ya watoto wakiwa hawafanyi vizuri, wenzake wakamcheka na kumwita majina ya kuumiza kama mjinga, mbumbumbu, huamua kukaa nyumbani.
“Baadhi ya watoto hawana uwezo wa kuhimili kuchekwa inachangia kuwapo kwa watoto wanaoacha shule.Kukosa mahitaji muhimu nayo ni moja ya changamoto inayofanya baadhi ya watoto kukosa mahitaji muhimu,’ anasema na kuongeza:
“Tunajua elimu ni bure kuanzia ngazi ya msingi na sekondari lakini kuna vitu mtoto anapaswa kuwa navyo kama kalamu, begi, madftari, watoto. Kuna baadhi ya michango pia wanashindwa kupata akifika shuleni anachapwa mwingine anaambiwa leta hela ya mlinzi anafukuzwa akiomba nyumbani anaambiwa aache hakuna hela.’’
Zaida anaungwa mkono na mwalimu mstaafu Nazaleth Mwenga, anayesema baadhi ya mikoa ina idadi kubwa ya watoto wanaoolewa katika umri mdogo, jambo linalohitaji kufuatiliwa kwa ukaribu na utaratibu mzuri uwekwe katika kukabiliana na hali hiyo.
“Mikoa kama Katavi, Mwanza, Simiyu inakaliwa sana na jamii ya Wasukuma, ambao ni ni kawaida kumuozesha binti akiwa na umri mdogo, elimu kubwa inahitajika kwao ili kuhakikisha wanaachana na mila hii,” anasema.
Anasema baadhi ya wazazi pia hawana mwamko wa elimu jambo ambalo linafanya ufuatiliaji wa maendeleo ya watoto wao kuwa mgumu, hali inayofanya wao kushindwa kujua kama watoto wao walifika shuleni kama inavyotakiwa, walijifunza na kufanya kinachotakiwa.
“Hakuna ufuatiliaji wa kutosha wa mzazi na hakuna mawasiliano kati ya mzazi na mwalimu na baadhi wanakimbia vikao au kujua maendeleo ya mtoto shuleni wakiogopa kudaiwa michango mbalimbali. Kama hakuna usimamizi wa mzazi na mwalimu mtoto hupotea hapo katikakati na a mwishowe anaacha shule,” anasema Mwenga.
Kuhusu mimba za utotoni ambazo zimezungumzwa na Mwenga, utafiti wa afya ya uzazi na mtoto pamoja na viashiria vya malaria Tanzania kwa mwaka 2022 (TDHS- MIS) unaonyesha, Tanzania imefanikiwa kupunguza mimba hizo kwa asilimia tano ndani ya miaka mitano ikiwa ni sawa na asilimia moja kwa mwaka.
Hiyo ni baada ya wastani wa mimba za utotoni kufikia asilimia 22 mwaka 2022, ikilinganishwa na asilimia 27 katika utafiti wa mwaka 2015/2016.
Ripoti inautaja Mkoa wa Songwe kuongoza kwa mimba za utotoni kitaifa ukiwa na asilimia 45, Ruvuma 37, Katavi asilimia 34, Mara asilimia 31 na Rukwa asilimia 30.
Katavi inaingia kwa mara nyingine, lakini ikiwa na kiwango pungufu kutoka asilimia 45 ikilinganishwa na utafiti wa mwaka 2015-2016.
Mbali na mimba, ndoa kwa wasichana nayo ni moja ya changamoto, ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi anasema ni moja ya sababu zinazokwamisha kufikia usawa wa kijinsia hasa katika upande wa elimu.
Anasema takwimu zinaonyesha chini ya theluthi moja ya wasichana wanaomaliza elimu ya msingi , hawamalizi elimu ya sekondari kutokana na vikwazo kadhaa vikiwamo ndoa na mimba za utotoni.
“Msichana mmoja kati ya watatu, anaolewa kabla ya kutimiza miaka 18 na mmoja kati ya wanne tayari ni mama kabla ya kufikisha miaka 18. Wasichana kuacha shule, kupata mimba na ndoa za utotoni vina uhusiano wa moja kwa moja. Pindi msichana anapopata mimba, ni vigumu kwake kuendelea na masomo na mara nyingi huishia kuolewa akiwa bado mdogo,” anasema.
Akizungumzia athari za mdondoko wa wanafunzi katika uchumi, mtaalamu wa biashara, Dk Donath Olomi anasema mara zote msingi wa uchumi wa nchi ni watu, hivyo ukiwa na nchi ambayo watu wake hawajapata eimu sahihi ni tatizo kimaendeleo.
Hiyo ni kwa sababu nchi inakuwa haina rasilimali watu ya kutosha inayoweza kujenga uchumi kupitia shughuli mbalimbali zinazohitaji ujuzi.
“Kitendo cha watu kuacha shule kinaashiria kuna tatizo katika mfumo wa malezi na elimu ambayo itakuwa na athari kubwa katika uchumi. Wakiacha shule unakuwa na watu ambao hawajaelimika sawasawa na wanakosa stadi muhimu za kufanya kazi inapohitajika,” anasema.
Pia kuacha shule kunaongeza idadi ya wategemezi hali inayotajwa kuwa na athari si katika uchumi pekee bali pia katika usalama wa nchi, kwani baadaye wanaweza kuwa chanzo cha kuvuruga amani kutokana na kufanya shuguli zinazohatarisha usalama wa raia na mali zao.
Ofisa Elimu mkoa wa Mwanza, Martine Nkwabi anasema zipo jitihada mbalimbali zinazofanywa na mkoa huo katika kukabiliana na utoro wa ngazi zote.
Anasema wanatambua kuwa asilimia 60 ya utoro husababishwa na familia anayotoka mtoto, asilimia 25 ikichangiwa na shule na asilimia 15 husababishwa na tabia ya mtoto.
“Kama mkoa umekuwa ukifanya jitihada kuondoa sababu za utoro zinazosababishwa na shule ikiwemo kutoa adhabu mbaya kwa watoto zinazofanya watoto kukimbia shule, hivyo tuliziagiza menejimenti za shule adhabu zinazotolewa ziendane na kosa,” anasema.
Mbinu nyingine inayotumika kudhibiti utoro katika mkoa huo ni kutumia watendaji wa kata kwa shule za sekondari na watendaji wa kijiji kwa shule za msingi.
“Hawa wamekuwa wanasimamia sana suala la watoto kwenda shule, mzazi kama umeandikisha mtoto ni lazima mtoto aende shuleni na asipoenda anahojiwa,”
Anasema suala hilo limeleta mabadiliko chanya katika wilaya za Misungwi, Kwimba, Buchosa ambapo watendaji wa kata huita wazazi na kuwaamuru kutoa baadhi ya vitu kama fidia kwa sababu watoto wao wameshindwa kwenda shule.
Pia wamekuwa wakihamasisha wazazi kupata watoto kulingana na uwezo wa kulea, ili waweze kuwatimizia mahitaji yao muhimu sambamba na kuwafundisha wazazi umuhimu wa elimu.
Katika kukabiliana na suala hili, Ofisi ya Rais – Tamisemi, kupitia bajeti ya mwaka 2025/2026 inasema imekamilisha uboreshaji na kuanza matumizi ya mfumo wa taarifa za shule unaosaidia kupata taarifa za shule kwa wakati.
Mfumo huo utasaidia kufuatilia maendeleo ya wanafunzi kimasomo, kung’amua vihatarishi vya utoro kwa wanafunzi vinavyoweza kusababisha wanafunzi kuacha shule.
“Hivyo kupitia mfumo huu utawezesha walimu kuchukua hatua mapema. Mfumo huu unatumika katika shule zote za umma na zisizo za umma nchini katika ngazi ya elimu msingi na sekondari,” anasema Waziri wa Tamisemi, Mohammed Mchengerwa
0 Comments:
Post a Comment