Mara nyingi inapotokea uchumi umeyumba au uchumi mbovu kunakuwa na idadi kubwa ya biashara kuweza kuyumba na zingine kuweza kufa kabisa. Hali hii hupelekea watu hasa wafanyabishara kuanza kupata tabu kwa kuyumba kiuchumi pia.
Ndio maana kabla hujafanya biashara unashauriwa kufanya utafiti wa kutosha na kuangalia ni biashara zipi ambazo zina mahitaji mengi au zinaweza zikadumu kwa muda mrefu pasipo kuteteleka au kufa kabisa hata kitokee kitu gani.
Pegine unajiuliza kweli kuna biashara ambazo haziwezi kufa? Katika mazingira ya kawaida unaweza ukakataa ukasema kwamba, kila biashara inaweza kufa. Lakini hapa leo nataka ni kukuonyesha biashara chache tu ambazo haziwezi kufa.
Katika makala hii, biashara hizo sitazichambua kwa kina bali nitakuonyesha tu mwanga au njia kisha utatafakari na kuangalia ukweli na uhalisia wa biashara hizo ambazo zinafanywa kwa vizazi na vizazi, na zinaleta mafanikio kwa wengi.
Kwa mtu ambaye ameamua kufanya biashara hizi na akabobea kweli, ni ngumu sana kuweza kumtoa kwa sababu zinalipa, labda wewe mwenyewe uamue kwamba sasa siwezi kuifanya tena biashara hii, ukaamua kukaa kwa kubweteka.
Lakini biashara ambazo nakwenda kukushirikisha hapo ni biashara ambazo zinafanyika katika mazingira yoyote yale. Zinafanyika kijijini na zinafanyika mjini, lakini ni biashara ambazo hazichagui kitu ilimradi tu wewe uamue kufanya kwa ufanisi na utafanikiwa.
Biashara ambazo haziwezi kufa au hata kama zikifa ndio zitakuwa za mwisho ni biashara za vyakula kama vile unga wa sembe, unga wa ngano, mchele, mafuta ya kula, sukari, maharage, dagaa, pamoja na chumvi. Hizi ni biashara ambazo zinadumu sana.
Ukiangalia hivi ni vitu ambavyo vinagusa matumizi ya watu ya kila siku. Hakuna siku ambayo itapita pasipo watu kufanya matumizi ya hivi vitu. Kila siku kwa mfano, unga eidha uwe wa sembe au wa dona unahitajika sana kila siku.
Watu wenye mashine au wanaojihusisha na biashara hii kwa mfano ya uuzaji wa unga wanajua ni biashara ambayo haiwezi kudorola sana, ni biashara ambayo ipo wakati wote, iwe njaa au kusiwe na njaa lazima watu wale.
Ni jukumu lako wewe kuangalia kwa mfano ni kipindi gani mahindi yanapatikana kwa urahisi na kusaga ili kupata unga huo na kuusambaza mtaani. Kuuza ni lazima utauza hata bila kujali kama utauza kwa faida ndogo au kwa faida kubwa.
Mbali na unga wa sembe ukiangalia upande mwingine maharage nayo, yanatumika sana kwenye familia zetu karibu kila siku na uzuri wake yapo maeneo mengi ambayo maharage haya yanapatikana kwa bei nafuu hususani hasa kipindi cha mavuno.
Unaweza ukanunua na kuyauza moja kwa moja au ukasubiri kipindi yakiadimika ukaanza kuyauza moja kwa moja na ikakusaidia kupata pesa. Uzuri soko lake liko wazi ukizingatia familia nyingi, zinatumia maharage kila siku.
Hali hiyo hiyo ndio inayoenda mpaka kwenye sukari, dagaa, mafuta ya kula, halikadhalika na ngano. Ni biashara ambazo zinawalaji wengi. Na watu wengi wametoka kupitia biashara hizo na kuwa na pesa nyingi sana.
Ukiwauliza watu wenye maduka ya reja reja ambayo yanauza vitu mchanganyiko, watakwambia vitu vinavyoendesha duka la reja reja au roho ya duka la reja reja ipo kwenye hivyo vitu na ndivyo vyenye faida.
Kama utaamua kufanya, kwa sababu pia wengi wanafanya, ni jukumu lako wewe kuingia na kufanya kwa akili, au kuongeza kitu cha ziada ili ufanye kwa ufanisi ikiwa ni kuanzia kwenye vifungashio na hilo litakusaidia kupata wateja wengi.
Kumbuka sijasema kwamba biashara hizi hazina changamoto. Kila biashara ina changamoto zake, lakini hata hivyo ni biashara ambazo walaji wake ni wengi na wanapatikana kila siku.
Mpaka hapo angalau umepata mwanga wa kile ambacho nilikuwa nataka kukuonyesha biashara ambazo haziwezi kufa au hata kama zikifa zitachukua muda mrefu sana kudondoka. Usichelewe kuchukua hatua, ndoto zako zinawezekana.
0 Comments:
Post a Comment