Kaimu kocha Mkuu wa Simba Masudi Djuma amewataka mashabiki wa timu hiyo kuwa na utulivu baada ya kufungwa na Azam FC jana kwenye mchezowa fainali ya kombe la Kagame.
Akizungumza baada ya mchezo huo ambao Azam FC iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kutwaa taji hilo, Djuma ametetea uamuzi wake wa kuwatumia wachezaji wapya na wale waliokosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Simba.
Amesema uamuzi huo utainufaisha Simba kuelekea kuanza kwa msimu mpya wa ligi kuu ya Vodacom 2018/19.
"Mimi ndiye niliyetoa ruhusa kwa baadhi ya wachezaji waliocheza sana wapumzike. Tumetoka kwenye ligi, tuemeenda kushiriki michuano ya SportPesa. Siku chache baadaye tumeingia kwenye mashindano haya ya Kagame" Djuma aliwaambia waandishi wa habari jana.
"Wachezaji ni binadamu lazima wapumzike ili waweze kurejesha afya zao. Lakini pia uamuzi huu umetusaidia kuona uwezo wa wachezaji ambao wengine hawakuwa wakipata nafasi kwenye kikosi cha kwanza"
"Baada ya mashindano haya tunaweza kufanya uamuzi sahihi juu ya yupi abaki, na yupi aondoke lengo likiwa kukiimarisha zaidi kikosi chetu."
Naye Mkuu wa Idara ya habari ya Simba Haji Manara ameunga mkono kauli iliyotolewa na kocha Djuma na kuwataka mashabiki wa timu hiyo wawe na imani kwa benchi lao la ufundi.
"Kabla ya kagame cup tuliitisha press conference na kuwaeleza Watanzania kikosi kitachotumika na kwa nini kuna wachezaji hawatatumika," Manara ameandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.
"Tuliwaeleza pia faida za kuwatumia wachezaji wengine hususan wale wapya na ambao hawakupata playing times ndefu last season.
"Sote tunakumbuka zile lawama za baadhi ya wachezaji kutokucheza. Leo tumeona faida yake. Yupo mtu atataka Kazimoto aachwe?au Rashid Juma asiwemo katika team?
"Kuna faida kubwa ya uamuzi waliofanya benchi la ufundi na hakika utalipa. Najua baadhi yenu ni ngumu kuelewa ila kupanga ni kuchagua na chaguo lao ndio uamuzi sahihi ambao soon mtapongeza.
"Nawakumbusha, msisahau tulifungwa na kagera Sugar tukiwa na kikosi kamili. Huo ndio mpira. Pengine tungeweza kuwa nao wote labda hata fainali tusingefika.
"Tafadhalini, tujitahidi kuuelewa mpira kabla ya kuushabikia," ameandika Manara.
0 Comments:
Post a Comment