Saturday, 14 July 2018

Simba yamnasa Dilunga

Simba imefanikiwa kunasa saini ya kiungo wa Mtibwa Sugar Hassani Dilunga ambaye jana amesaini mkataba wa miaka miwili kutua Msimbazi.

Dili la Dilunga na mabosi wa Simba lilikamilishwa kwa usiri mkubwa jana kulingana na gazeti la Mwanaspoti

Kulinganga na gazeti hilo, mmoja wa viongozi waandamini wa Simba alikiri kuwa Dilunga amesaini mkataba wa miaka miwili na wamemalizana naye kila kitu.

“Kwanza hayakuwa mazungumzo marefu kwani tulizungumza hapo awali, alikuja kusaini tu mkataba ambapo tumempa kila alichohitaji na tumeamua kufanya kimya kimya kwani, anatafutwa sana,” alisema kiongozi huyo.

Dilunga alikuwa mchezaji bora wa michuano ya Kombe la FA ambapo, Mtibwa Sugar walichukua ubingwa kwa kuifunga Singida United bao 3-2, alisema amemalizana na Simba msimu ujao atakuwa mchezaji wa timu hiyo.

Alisema haitakuwa kazi rahisi kwake kwani mpaka Simba wamemsajili wameona anaweza kuisaidia timu hiyo hivyo, anataka kulinda na kuongeza kiwango chake ili kufanya zaidi ya alivyo sasa.

“Natambua nakwenda kwenye timu yenye wachezaji wenye viwango vya juu hasa eneo la kiungo, jambo ambalo linanipa mzuka wa kujituma ili kushinda changamoto hiyo na kuaminiwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara,” alisema.

“Nipo tayari kushindana na changamoto zote pale Simba kwa kuwa nataka kucheza na Simba ni timu kubwa,” alisema Dilunga.

Mkurugenzi wa Mtibwa, Jamal Bayser alisema kama mambo yote yakikalimilika wataweka wazi ingawa kila kitu kinakwenda sawa na lolote linaweza kuwepo kati yao na Simba.

“Nadhani tusubiri kwanza kidogo kuna mambo yakikamalika nitasema kwamba, Dilunga ataendelea kuwepo Mtibwa au kwenda timu nyingine, kwa sasa hakuna lolote ambalo naweza kusema,” alisema Bayser.

Kocha wa Simba Mrundi, Masoud Djuma kabla ya usajili huo kukamilika alipendekeza viungo wawili ambao ni Dilunga ambaye Simba wamemnasa na Feisal ‘Totoo’ aliyewaponyoka dakika za mwishoni na kutua Yanga.

“Nilimuona Fei Toto ni kiungo mzuri na nilitegemea viongozi kuwa watakuwa wamekamilisha usajili wake, lakini alituambia amesaini katika timu nyingine,” alisema.

“Kwangu ningefurahi sana kama Fei Toto angekuja kucheza na viungo au wachezaji wa Simba nadhani angefika mbali kisoka, lakini kama imeshindikana na kaamua kwenda timu nyingine yote sawa.

“Nilipendekeza viungo wawili na baada ya kumkosa Fei Toto nadhani viongozi watakuwa wamefanya kazi sahihi na mapendekezo thabiti kabisa ya kumsajili Dilunga kwani, ni miongoni mwa mapendekezo yangu,” alisema Djuma.

“Dilunga ni kiungo mzuri ambaye ataongeza kitu katika timu yetu kwani ilikuwa lazima tusajili kiungo mzuri mshambuliaji wa kariba yake na kumpata kwake niwapongeze viongozi wanafanya kazi kama inavyotakiwa,” aliongezea Djuma

0 Comments:

Post a Comment