Mshambuliaji mpya wa Simba, Marcel Kaheza amesema haogopi ukubwa wa majina wa mastaa wanaocheza namba moja ndani ya kikosi hicho, badala yake anaongeza juhudi ya mazoezi ili ajihakikishie namba katika kikosi cha kwanza kwa msimu ujao.
Kaheza alisajiliwa na Simba, akitokea Majimaji ya Songea, anakiri uwepo wa washambuliaji Emmanuel Okwi, John Bocco na Meddie Kagere ni changamoto kwake, lakini haimfanyi awahofie na kujiona hana lake msimu ujao.
"Hii ni kazi inayohitaji ushindani, ukikaa na kuanza kutafakari majina na ustaa wao huwezi kufanya lolote na mwanaume halisi haogopi changamoto za kukabiliana na kila hali.
"Uwezo wao unanifanya nijitume kwa bidii, kwani kabla sijasaini nilijua kuna wachezaji Simba ambao kazi yao ipo imara na wanajua kupambana na ndio maana niliamua kukubali kuwatumikia ili kuingia kwenye ushindani," alisema Kaheza.
Kaheza alisema tayari amepata picha ya nini atakifanya katika msimu ujao, baada ya kucheza Kombe la Kagame ambalo lilikuwa na wachezaji wazoefu atakaokuwa nao msimu ujao.
"Mfano mzuri ni huyo Kagere kwa hiyo nilikuwa najifunza ana vitu gani vinavyomfanya awe bora, kwa hiyo nipo tayari kwa ajili ya ushindani siwezi kuwa na hofu itakayonifanya nishindwe kuthubutu kuingia kwenye ushindani wa namba," alisema Kaheza.
0 Comments:
Post a Comment