Sunday 22 July 2018

Kikosi ghali duniani

LIVERPOOL wamevunja kibubu na kuinasa saini ya Mbrazil Alisson kutoka AS Roma kwa dau la pauni mil 65, uhamisho uliomfanya Allison kuwa kipa ghali zaidi duniani.

Mbali na uhamisho huo, yapo madili yaliyowahi kutikisa dunia kwa timu kumwaga fedha za kutosha kunasa saini za mastaa. Hii hapa ndiyo ‘First Eleven’ ghali duniani.

Alisson (Roma kwenda Liverpool pauni mil 65)

Kila mmoja anaamini Mbrazili huyu anakwenda kutibu tatizo sugu la Liverpool.

Ametokea Roma na mashabiki wa Liverpool watakuwa na furaha kubwa kwa kuinasa saini ya kipa huyu aliyemfanya nyanda wa Manchester City, akose namba katika timu ya taifa ya Brazil.

Ndiye kipa ghali zaidi duniani kwa sasa na ujio wake unawaweka kwenye wakati mgumu makipa wawili wa Liver, Simon Mignolet na Loris Karius.

Benjamin Mendy (Monaco kwenda Man City, pauni mil 51.75)

Mcheshi asiyeishiwa vituko. Ni ngumu mno kumchukia Mendy. Beki wa kushoto mwenye kiwango kikubwa sana duniani, licha ya kukosa namba kwenye kikosi cha kwanza cha Pep Guardiola.

Na hii ni kutokana na jeraha la msuli alilopata Septemba mwaka jana. Karibu msimu mzima wa 2017-18, Mendy alikuwa mbali na uwanja.

Akiwa fiti, Mendy alikuwa mchango mkubwa katika kikosi cha Monaco kilichobeba taji la Ligue 1 na kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, msimu wa 2016-17.

Usitarajie kuendelea kumuona Delph akicheza beki wa kushoto kwenye kikosi cha Man City, Mendy akiwa fiti.

Virgil van Dijk (Southampton kwenda Liverpool, pauni mil 70.1)

Kama ilivyo kawaida ya Liverpool. Mara hii tena walipiga hodi Southampton na kumnyakua beki kisiki Virgil van Dijk kwa dau la pauni mil 70.

Awali ilionekana kama kamari kubwa kucheza na Liverpool, lakini kwa kipindi kifupi tu ndani ya Anfield, VVD amethibitisha ubora wake.

Golini ukiwa na Alisson na beki wako wa kati ni Van Dijk, bila shaka msimu huu tutaishuhudia Liverpool bora kabisa chini ya Jurgen Klopp.

Aymeric Laporte (Atletic Bilbao kwenda Man City, pauni mil 58.5) 

Pep Guardiola alifanya uamuzi wa haraka wa kumsajili Laporte, baada ya kukabidhiwa mikoba ya kukinoa kikosi cha Man City.

Beki huyu wa kimataifa kutoka Hispania ameendelea kuzoea taratibu mazingira ya soka la England, hivyo kuna uwezekano mkubwa msimu huu akapata namba kwenye kikosi cha kwanza.

Ushirikiano wa Laporte na John Stones ndicho kitu ambacho Pep Guardiola ameendelea kutamani kuona kikitokea katika kikosi chake.

Kyle Walker (Tottenham kwenda Man City, pauni mil 47.5)

Tottenham walifanya kila waliloweza, lakini mwisho wa siku beki huyu raia wa England alitimka na kusaini Manchester City.

Uamuzi wenye faida kwa Walker. Msimu wake wa kwanza akiwa na City amefanikiwa kubeba Kombe la Premier League na kuwaacha Tottenham wakiendelea kusotea taji hilo.

Mbali na kucheza kama beki wa pembeni, Walker pia ana uwezo wa kucheza beki wa kati kama alivyotumika kwenye Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha England.

Paul Pogba (Juventus kwenda Man United, pauni mil 94)

Usajili uliotawaliwa na maneno, mitazamo tofauti tofauti duniani ni huu wa Paul Labile Pogba kutoka Juventus kwenda Man United.

Baada ya kucheza kwa mafanikio makubwa chini ya makocha Antonio Conte na Massimiliano Allegri kule Turin, Jose Mourinho hakusita kuvunja kibubu na kumrejesha Pogba Old Trafford.

Mashabiki wengi wa United wana imani baada ya Pogba kubeba taji la dunia kule Russia, atarejea Old Trafford akiwa moto na kuwasaidia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England.

Philippe Coutinho (Liverpool kwenda Barcelona, pauni mil 112.5)

Liverpool waliendelea kusisitiza kuwa hawako tayari kufanya biashara ya kumuuza Coutinho.

Lakini baada ya Neymar kuondoka Camp Nou na kwenda PSG, Barcelona hawakuwa na njia nyingine zaidi ya kurejea kwa Coutinho.

Katika dirisha dogo la usajili Januari mwaka huu, Barca wakalipa pauni mil 112.5 kwa Liverpool na kumbeba Coutinho.

Uwezo wa Coutinho ndio umewafanya Barca kukubali kumwachia kiungo wao mkongwe, Andres Iniesta, kuondoka Camp Nou. Tayari viatu vyake vimepata mrithi.

James Rodriguez (Monaco kwenda Real Madrid, pauni mil 67.5)

Baada ya kung’ara kwenye Kombe la Dunia 2014, hakukuwa na namna Monaco wangeweza kumzuia James Rodriguez asiondoke.

Kama ilivyo kwa Real Madrid, sera ya Galactico ikatumika kumvuta Rodriguez kwa uhamisho uliogharimu pauni mil 67.5.

Lakini mambo hayakwenda kama ilivyotarajiwa. Maisha ya James ndani ya Bernabeu hayakuwa mazuri, hali iliyopelekea kutolewa kwa mkopo katika klabu ya Bayern Munich.

Neymar (Barcelona kwenda PSG, pauni mil 199.8)

Hakuna aliyetarajia usajili huu ungekuja. PSG wakiwa na fungu la kutosha waligonga hodi Camp Nou na kuibeba saini ya Mbrazil Neymar.

Ndoto za Neymar zilikuwa ni kubeba Ballon d’Or na hilo lilionekana kuwa gumu kutimia kama angeendelea kucheza Barcelona akiwa na Lionel Messi.

Yuko PSG. Kwa lolote litakalotokea baadaye, halitaondoa ukweli kuwa usajili huu uliibadilisha dunia moja kwa moja.

Cristiano Ronaldo (Real Madrid kwenda Juventus, Pauni mil 105)

Ilipoonekana Ronaldo amekinai mafanikio na Real Madrid na sasa anahitaji changamoto mpya, Juventus waliibuka wakiwa na dau la pauni mil 105.

Uhamisho sahihi kwa Real Madrid, Juventus na Cristiano Ronaldo mwenyewe. Mengine ni kusubiri kuona yakitokea.

Kylian Mbappe (Monaco kwenda PSG, Pauni mil 121) 

PSG walimtoa Monaco kwa mkopo na hii ikiwa njia ya kukwepa rungu la Fifa, katika sheria ya matumizi na mapato (Financial Fair Play).

Ubora wa Mbappe umeonekana akiwa na Ufaransa kwenye Kombe la Dunia 2018. Ni kijana bora kweli kweli.

Akiwa na miaka 19, ameweka rekodi ya kuwa kinda wa pili kufunga bao katika fainali ya dunia. Lakini pia Mbappe ni mchezaji bora chipukizi wa Kombe la Dunia 2018.

0 Comments:

Post a Comment