Thursday 19 July 2018

Simba yamtambulisha kocha mpya


Uongozi wa klabu ya Simba umemtangaza rasmi kocha wao mpya, Mbelgiji Patrick Aussems, tayari kuanza kazi ya kuiandaa timu kuelekea mashindano ya Ligi Kuu Bara.

Simba wameingia makubaliano ya mkataba wa mwaka mmoja na Aussems akiwa anachukua mikoba ya Mfaransa, Pierre Lechantre ambaye alimaliza muda wake.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya mabosi wa Simba kugoma kumuongezea mkataba Lechantre ambaye alipewa timu kwa muda wa miezi sita pekee na baada ya kumalizika wakaacha naye.

Aussems amesaini mkataba huo mbele ya Makamu Rais wa klabu hiyo, Salim Abdallah maarufu kama Try Again, sambamba na Kaimu Makamu wa Urais, Idd Kajuna pamoja na Waandishi wa Habari.

Kocha huyo amewahi kuzinoa timu kadhaa za Afrika ikiwemo AC Leopards ya Congo, KSA Cameroon ya Cameroon, ES Troyes AC ya Ufaransa na zingine zilizopo  je ya Afrika.

Simba wamefikia hatua ya kumpa mkataba wa mwaka mmoja baada ya kuridhishwa na CV zake hivyo kuona anastahili kukinoa kikosi hicho ambacho kimeshiriki michuano ya SportPesa Super CUP na KAGAME bila ya Kocha Mkuu.

Wakati Aussems akimwaga wino, kikosi cha Simba kinatarajiwa kusafiri kuelekea nchini Uturuki kwa ajili ya kambi ya wiki mbili kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa ligi unaotaraji kuanza Agosti 22.

0 Comments:

Post a Comment