Thursday 19 July 2018

Wawili waongezwa kesi ya vigogo wa Simba

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeagiza upande wa mashitaka kubadilisha hati katika kesi ya utakatishaji fedha inayowakabili, Rais wa klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake Godfrey Nyange Kaburu.

Agizo hilo limetolewa Jumatano, Julai 18, mwaka huu na hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya mwendesha mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU ), Leonard Swai kudai kuwa kesi hiyo imekuja kwaajili ya kutajwa na kwamba mahakama ilitoa amri ya kubadilisha hati ya mashitaka na kuongeza washitakiwa wawili ambao ni Mwenyekiti wa Usajili wa Simba, Zacharia Hans Poppe na Franklin Lauwo.

Wakili Swai amedai kuwa jukumu la kubadilisha hati liliachwa kwa wakili wa Serikali, Shadrak Kimaro baada ya yeye kusafiri kwenda Moshi na sasa amerejea kuja kukamilisha kazi hiyo huku akiiomba Mahakama siku saba ili kukamilisha mabadiliko ya hati ya washitakiwa.

Kwa upande wa wakili wa utetezi, Nehemiah Nkoko alidai kuwa hati ya mashitaka iliyotakiwa kufanyiwa mabadiliko ni ya watu wanne na wenyewe wapo wawili hivyo wanaomba wafanye haraka kubadilisha hati hiyo.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 26, mwaka huu itakapotajwa tena.

Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashitaka matano ya uhujumu uchumi ikiwamo, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo na kutakatisha fedha dolla za kimarekani 300,000 ambazo ni sawa na sh. Millioni 600 za kitanzania .

April 30, mwaka huu mahakama hiyo iliwaongeza Hans Poppe na mkandarasi wa uwanja wa klabu hiyo, Franklin Peter Lauwo na kuagiza wakamatwe na kufikishwa mahakamani jambo ambalo limelalamikiwa na wakili Swai kuwa wamewatafuta tangu mwezi Machi bila mafanikio yoyote na kuomba hati ya kuwakamata. 

0 Comments:

Post a Comment