Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la soka nchini (TFF) imekubaliana kupitisha mfumo wa Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza(FDL)ambapo kuanzia msimu ujao FDL itachezwa katika makundi mawili yenye timu 12 na timu 1 kutoka kila kundi itapanda kwenda Ligi Kuu.
Timu ya pili na ya tatu katika kila kundi zitacheza mtoano kwa mechi za nyumbani na ugenini na washindi katika mechi hizo watacheza na timu iliyoshika nafasi ya 17 na 18 katika Ligi Kuu kupata timu mbili zitakazocheza Ligi Kuu huku timu mbili za nafasi ya 19 na 20 zikishuka daraja.
Timu hizo mbili za Ligi Kuu zilizoshika nafasi ya 17 na 18 kama zitapoteza michezo yao zitashuka Daraja kuungana na zilizoshika nafasi ya 19 na 20.
Nia ya dhati ni kuongeza ushindani wa Ligi Kuu,FDL na SDL.
Vilevile Kamati ya Utendaji imekubaliana kuchezwa kwa mashindano ya Taifa Cup kati ya Mwezi Juni na Julai 2019 huku pia ikipitisha kuchezwa kwa mashindano ya Vijana U15 katika mtindo uliokuwa unatumika kwenye Copa Coca Cola wakati yale ya U17 yenyewe yatahusisha klabu za Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na Daraja la Pili kwa pamoja.
Nayo mashindano ya Kombe la Shirikisho yataanzia katika ngazi ya mkoa ambapo kila mkoa utakuwa na bingwa wake.
0 Comments:
Post a Comment