Kibaha. Wanachama wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Pwani wamedai kuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kucheleweshwa kwa malipo ya pesa za likizo, uhamisho, masomo pamoja na gharama za kufungasha mizigo kwa wastaafu.
Mbali na hilo walimu hao wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kutowaacha maafisa Elimu wa Halmashauri kukaa muda mrefu kituo kimoja cha kazi kwani hali hiyo imekuwa ukisababisha baadhi yao kufanya kazi kwa mazoea ikiwemo kuminya stahiki za Walimu.
Wametoa Kilio hicho leo Jumamosi Mei 27, 2023 kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Rashid Mchata aliyekuwa mgeni rasmi kwenye kikoa cha Baraza la CWT Mkoa wa Pwani kilichofanyika mjini hapa.
“Tushauri ikiwezekana Maafisa Elimu wawe wanabadiliishiwa vituo vya kazi ndani ya Mkoa,” imesema sehemu ya risala yao iliyosomwa na Katibu wa CWT mkoani humo.
Kuhusu pesa za miradi zinazopelekwa shuleni kwaajili ya ujenzi, Walinu hao wameishauri Serikali kuweka utaratibu wa kuwapa elimu Wakuu wa Shule Ili wapate uelewa wa kutosha kabla ya kuanza matumizi na hivyo kuwasaidia kutoingia matatani kwa kutofuata taratibu na miongozo ya pesa hizo.
Naye Mwenyekiti wa Chama hiyo Pwani, Doughaus Mhini amesema kuwa changamoto nyingine kwa sasa ni kuhusu mikataba ya utendaji kazi ambayo inawachukulia muda kuiandaa na wakati mwingine kujikuta wanaingia migogoro na Serikali hasa pale wanapopata uhamisho jambo ambalo ameomba lingaliwe namna ya kuliboresha.
Akizungumzia kuhusu changamoto hizo Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Rashid Mchata amesema kuwa Serikali imeendelea kuzifanyia kazi kulingana na hali halisi inayokuwepo kwa wakati husika, hata hivyo amewata kuwa wavumilivu.
“Nimesikia changamoto mlizowasilisha, yote yanafanyiwa kazi lakini na mimi pia napenda kuwashauri jitahidini kuwa wabunifu kulingana na fursa zilizopo kwenye maeneo mnakofanyia kazi na si kutaka kuhamahama kutokana na mazingira,” amesema.
Amesema kuwa ubunifu wanaopaswa kufanya ni ule unaoleta matokeo chanya na maendeleo ya Elimu pamoja na miundombinu kwenye Shule zao kwani kufanya hivyo watakuwa wanapandisha wasifu binafsi huku jamii ikinufaika.
“Lakini lingine manalopaswa kulikumbuka ni kwamba ajira zina mwisho hivyo jitahidini kujiwekea akiba kwa njia mbalimbali, wekezeni ili hata mkistaafu muendelee na maisha mazuri,” amesema.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa wa Chama hicho Herbert Ngimi amesema pamoja na changamoto zilizopo lakini Serikali imeonyesha kuwajali walimu hasa kwa kuwapandisha madaraja na kuwaongezea kiwango cha mishahara hivyo wanaishukuru kwa hatua hiyo kwani imewapa morali wa kufanyakazi
0 Comments:
Post a Comment