Saturday, 27 May 2023

Ushirikina Katika Michezo


HADI miaka ya karibuni kandanda ilihesabika kuwa mchezo unaohusisha wachezaji, viongozi na mashabiki.
Lakini siku hizi, mbali ya wachezaji 11 wanaoteremka uwanjani pamekuwapo wachezaji wengine nje ya uwanja ambao inasemekana ati kuwa nao wanacheza kwa kutumia kitufe.

Hawa ni wachawi na baadhi ya timu zimeajiri rasmi hawa wachawi ili kusaidia kupata ushindi.
Baadhi ya wachezaji mashuhuri duniani nao wanaajiri wachawi ili kuwasaidia wang’are na kubaki kuwa wachezaji nyota.
Kwa bahati mbaya ushirikina katika kandanda unaposimuliwa utasikia timu za Afrika za klabu na taifa ndio zinazohusika, lakini ukweli mambo haya siku hizi ni ya kawaida katika kila pembe ya dunia.

Hapa kwetu wachawi (au waganga) huchukuliwa na kubandikwa jina na Kamati ya Ufundi, lakini huo ufundi wao bado hauonekani kutusaidia kushinda katika mashindano ya kimataifa ya Afrika na dunia.

Katika kandanda wapo wachawi wanaosifika kuwa ‘kiboko’ na kugombaniwa na wachezaji, klabu na nchi.
Kwa mfano, baadhi ya wachezaji wa klabu za Ufaransa na timu ya taifa hilo wanadaiwa kumtegemea sana mchawi aitwaye Ibrahim, mwenye asili ya Senegal.
Ni kawaida unapofika nyumba kwake katika kitongoji cha Roissy-en-Brieje cha jiji la Paris, utakuta zaidi ya watu 30, wengi wakiwa viongozi wa klabu, wachezaji mashuhuri na wa Shirikisho la Kandanda la Ufaransa.

Wote hao wanatafuta mafanikio yao binafsi au timu wanazoziongoza kwa nafasi tafauti, kama za kocha au utawala.
Miongoni mwa kesi ya wachezaji na ushirikina iliyogonga vchwa vya habari mwaka jana ni ile kiungo maarufu, Paul Pogba juu ya uhusiano wake na Ibrahim.

Hapo kwanza, Paul Pogba alidaiwa kumtumia mdogo wake Mathias Pogba kuwasiliana na Ibrahim na baada ya kuona anatapeliwa na hapati mafanikio akaifanya kazi hiyo mwenyewe.
Katika sakata hili, Paul Pogba alidaiwa kumroga staa mwenzake wa timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe ili asifunike umaarufu wake na kuzusha mjadala mkali na shutuma nzito.
Hatimaye Paul Pogba alidai alimtumia mchawi Ibrahim amsaidie asijeruhiwe na sio kumuumiza Mbappe au mchezaji mwengine yeyote yule.

Pogba inasemekana alimlipa Ibrahim jumla ya dola 14 milioni za Kimarekani.
Katika mwaka 1997 klabu ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa ilikaribia kufilisika kwa kutumia fedha nyingi kuwalipa wachawi, wakiwamo waliotoka nchi za Afrika Magharibi.
Katika fainali za Kombe la Dunia 2002 zilizofanyika Korea na Japan, timu ya Senegal, The Lions of Terenga, iliambatana na Ngoy Lingueul Mbaye, kama mchawi wake aliyesaidiwa na jopo la wasaidizi.

Katika fainali hizo za 2022, Ghana ilikwenda na mchawi maarufu wa nchi hiyo, Nana Kwaku Bonsam,ambaye kazi yake kubwa ilikuwa kuhakikisha Ronaldo anaumia na asicheze pale nchi hiyo ilipopambana na Ghana katika kundi H.
Lakini badala yake Ronaldo alikuwa hashikiki na kuingoza Ureno katika ushindi wa 3-2.

Hapo kabla Bonsam alikiambia kituo cha radio cha Angel FM cha Ghana kwamba aliua mbwa wanne ili kutengeneza dawa maalum ya kishirikina ya kumdhibiti Ronaldo.
Katika fainali zile, Senegeal nayo ilidaiwa kuwatumia waganga wa kienyeji kumtibu mshambuliaji wake hatari Sadio Mane ambaye alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya goti aliyoyapata katika ligi ya Bundesliga ya Ujerumani siku chachache kabla ya kwenda Qatar kwa fainali za Kombe la Dunia.

Safari ya kugombea tiketi ya fainali za Kombe la Dunia za 1970, Australia ilipaswa kuifunga Zimbabwe (wakati ule ikiitwa Rhodesia) ili kufuzu, viongozi wa timu hiyo iliwalazimu kwenda Msumbiji kutafuta wachawi watakaowasaidia na wakampata mmoja aliyewapa mifupa ya binaadamu kuifukia karibu na goli watakaloanzia wapinzani wao.

Racing Club ni moja ya klabu maarufu ya Argentina. Kuanzia mwanzo wa miaka ya 1960 ilikuwa inafanya vibaya na kila msimu kuwa hatarini kuporomoka na kuchomoa dakika za mwisho.

Lakini hatimaye ilifanya vizuri na viongozi walidai walipata mabadiliko hayo baada ya mchawi wao kuwataka wawafukie paka weusi saba waliokufa karibu na uwanja na mara tu baada ya kufanya hivyo ndio wakaanza kupata mafanikio.
Katika mwaka 1983 mabaki ya paka hao yalifukuliwa katika ibada maalum iliyofanywa na kanisa Katoliki.

Karibu nchi zote za Afrika Magharibi, mbali ya kutegemea mafunzo maalum kutoka kwa mwalimu, lakini hutegemea zaidi mchawi na inasemekana nchi zinazoongoza kwa ushirikina katika kandanda katika ukanda huo ni Mali na Burkina Faso.
Katika nchi hizi hata timu za watoto wa chini ya miaka 10 wanapokuwa na mashindano basi huenda kwa waganga kupata msaada.

Katika nchi jirani ya Rwanda mambo ya ushirikina yamesheheni katika kandanda na hasa mahasimu wakuu, Mukura Victory na Rayon Sports. Uwanjani hutupwa mayai viza, mikojo ya wanyama, hirizi na vitu vingi vya ajabu.

Mashirikisho ya kandanda ya nchi nyingi siku hizi yametunga sheria kali za kudhibititi ushirikina ndani na nje ya uwanja.
Tanzania, TFF imekuwa ikizitoza faini timu ambazo zinafanya vitendo vinavyoashiria ushirikina na Yanga na Simba ni kati ya timu ambazo zimekumbana na adhabu hiyo mara kwa mara.

0 Comments:

Post a Comment