Saturday, 27 May 2023

Fei Toto Awashtua Wadau Wa Soka Nchini

KIUNGO Feisal Salum ‘Fei Toto’ amewashtua wadau wa soka nchini baada ya kutumia akaunti zake za mitandao ya kijamii kutembeza bakuli la kusaka fedha za kumpeleka Mahakama ya Usuluhishi la Kimataifa la Michezo (CAS) ili kuiburuza Yanga iliyoshindwa kumuachia licha ya kuvunja mkataba.

Fei aliingia kwenye mzozo na Yanga tangu mwishoni mwa mwaka jana alipotangaza kuvunja mkiataba kisha kuilipa klabu hiyo Sh 112 Milioni zikiwamo za miezi mitatu, lakini mabosi wa Yanga walimkomalia na kumrudisha fedha hizo kisha kumburuza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kupitia Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya TFF, ilibainika kwamba kiungo huyo mwenye mabao sita hadi sasa katika Ligi Kuu alivunja mkataba kienyeji na anaendelea kutambulika kama mchezaji halali wa Yanga na kupitia jopo lake liliomba marejeo ya hukumu hiyo na bado alikwama.

Wakati akisikiliziwa kama ataibukia klabu kama aliovyotakiwa na mabosi wake, ambao mapema juzi walitoa taarifa ya kuitwa kwa kiungo huyo kwenye Kamati ya Sheria na Nidhamu ya klabu kwa kuwa mtoro kazini sambamba na utovu mwingine wa nidhamu tangu alipoajiondoa Yanga kinyemela.

Inaelezwa pia kiungo huyo amezuia akaunti yake kupokea mishahara kuitoka klabu ya Yanga kwa karibu miezi minne sasa, huku akiwa haonekani kazini licha ya kuitwa na kutakiwa kuripoti kambini kuungana na wachezaji wengine.

Mara baada ya taarifa hiyo ya klabu ya Yanga, ndipo kiungo huyo naye akatoa taarifa katika mitandao ya kijamii akiomba kuchangiwa fedha ili aende CAS kuitafuta haki yake na tangazo hilo limepokelewa kwa hisia tofauti na wadau wengi wa soka ambao wameona kama mchezaji huyo anazingua.

“Tafadhali naomba unichangie ili nipate haki yangu itakayoniwezesha kutumikia kipaji changu na timu za taifa katika namna tofauti kwa manufaa yangu na taifa. Unaweza kulipia kwa lipa kwa namba au kwa namba ya simu,” inasomeka taarifa hiyo ya Fei Toto kutupia akaunti yake ya Instagram.

Baadhi ya mashabiki wamehoji sababu ya nyota huyo kuomba michango wakati alitakiwa kuwepo kazini na kuendelea kulipwa fedha kama kawaida na Yanga, huku wengine kudiriki kumchana wazi kwamba hawatamchangia kwa vile Fei hana sababu ya kuhitaji michango hiyo kuitoka kwao kwa sasa.

0 Comments:

Post a Comment