Saturday, 27 May 2023

Kocha Wa Yanga Aeleza Mikakati Ya Ushindi Kesho

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mtunisia Nasreddine Mohamed Nabi amesema ana matumaini ya matokeo mazuri baada ya maandalizi waliyofanya kwa ajili ya Fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika kesho dhidi ya USM Alger ya Algeria Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam. 
"Maandalizi tumeyagawa katika sehemu kuu tatu, ya kwanza ni utimamu wa miili ya wachezaji, pili ni kumjua mpinzani na tatu ni mbinu gani za kutumia kumkabili,"amesema Nabi katika Mkutano na Waandishi wa Habari leo kuelekea mchezo huo kesho Saa 10:00 jioni.
Lakini Nabi amesema wameumia kumkosa kiungo Mganda, Khalid Aucho ambaye kutokana na kukusanya jumla ya kadi sita za njano katika michuano hiyo atakosa mechi zote mbili za fainali Dar es Salaam kesho na Algiers Juni 3.
"Hakuna namna, ni suala la kikanuni. Tumezungumza naye na atakuwa na timu kwenye mechi zote mbili kwa ajili ya kuwahamasisha (wenzake) kupata matokeo mazuri,"amesema Nabi.
Hata hivyo, Mtunisia huyo amesema wanajivunia kuwa na mshambuliaji wa kiwango cha juu kikosi Afrika, Mkongo Fiston Kalala Mayele.
"Tuna bahati kuwa na Mayele kwenye kikosi chetu, ni mshambuliaji wa daraja la juu Afrika. Uzoefu wake pamoja na wachezaji wengine utakuwa msaada mkubwa kwetu kwenye hatua hii ya Fainali" 
Kwa upande wake beki Dickson Job amesema kwamba tayari maelekeo ya mambo ya kufanya ndani ya Uwanja, hivyo kazi imebaki kwao wao kama wachezaji kwenda kupambana ili washinde mechi hiyo.
"Watanzania waondoe uoga, nawaomba wajitokeze kwa wingi siku ya kesho na kushangilia kwa dakika zote. Vijana wao tuko tayari kwa ajili ya kupambana kuwapa furaha,"amesema Job anayeweza kucheza nafasi zote ulinzi, ukiondoa langoni.
Mechi hiyo itachezeshwa na refa, Jean-Jacques Ngambo Ndala atakayesaidiwa na Olivier Kabene Safar, wote kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zakhele Thusi Granville Siwela wa Afrika Kusini watakaokuwa wanakimbia na vibendera pembezoni mwa Uwanja kulia na kushoto.
Kufika hatua hii, Yanga iliitoa Marumo Gallants ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-1, ikishinda 2-0 nyumbani na 2-1 ugenini, wakati USM Alger iliitoa ASEC Mimosas ya Ivory Coast baada ya sare ya 0-0 ugenini na ushindi wa 2-0 nyumbani.

0 Comments:

Post a Comment