Tuesday 20 June 2023

Benki Kuu Yapiga Marufuku Malipo Ya Fedha Za Kigeni Nchini


Benki Kuu ya Tanzania imeukumbusha umma kuwa kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006 kinaelekeza kuwa shilingi ya Tanzania ndiyo fedha pekee ambayo inaruhusia kutumika nchini, hivyo hakuna Mtu au Kampuni yoyote inayoruhusiwa kuikataa kwa malipo yoyote halali na kwamba kitendo cha kukataa malipo kwa shilingi ya Tanzania ni kuvunja Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006.

“Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuukumbusha umma kwamba Serikali ilishatoa tamko kuhusu katazo la matumizi ya fedha za kigeni kwa Wakaazi wa Tanzania katika kulipia bidhaa na huduma nchini, tamko la kwanza lilitolewa mwezi Agosti 2007 na la pili mwezi Desemba 2017”

“Hata hivyo, katika siku za karibuni imebainika kuwepo kwa ukiukwaji wa tamko hilo, hivyo Benki Kuu inapenda kuukumbusha umma kwamba maagizo yaliyotolewa hapo awali kuhusu matumizi ya fedha za kigeni yanapaswa kuendelea kuzingatiwa kuwa bei zote hapa nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania, bei hizi zinajumuisha kodi za kupangisha ardhi, nyumba na ofisi, gharama za elimu, huduma za afya, vifaa tiba na vitendanishi, gharama za usafiri, lojistiki za bandari, vifaa vya kielektroniki na huduma za mitandao ya mawasiliano”

“Bei ambazo walengwa wake Wakuu ni Watalii au Wateja wasio Wakaazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni, bei hizi zinajumuisha gharama za hoteli, usafiri, gharama za viwanja vya ndege na viza kwa Wageni, usafirishaji kwenda Nchi za nje kupitia Tanzania na gharama za mizigo bandarini”

0 Comments:

Post a Comment