MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeelezwa kuwa Happiness Fredrick, aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kabla ya kunyongwa na anayedaiwa mpenzi wake, alimtumia mama yake ujumbe mfupi kwa simu kuwa alikuwa na wakati mgumu, hivyo wamwombee.
Inadaiwa kuwa Machi 18, 2019 Happiness alinyongwa na Idrisa Mwakabola baada ya kijana huyo kuhisi anasalitiwa kimapenzi na binti huyo. Inadaiwa alimwekea kidonge cha usingizi katika juisi kisha kumnyonga.
Baba wa marehemu, Fredrick Francis (51), mbele ya Jaji Ephery Kisanya, akitoa ushahidi wake mwishoni mwa wiki, alieleza namna siku ya tukio mtoto wake alivyotoka nyumbani na kumpata akiwa maiti huku akiwa ameacha ujumbe kwa wadogo zake.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Upendo Mono, Francis alidai kuwa siku hiyo ya tukio, binti yake alitoka nyumbani akielekea Stendi ya Ubungo kwa ajili ya kukata tiketi ili kurudi chuoni mkoani Dodoma.
“Saa 10 jioni mimi nikiwa katika shughuli zangu, alinipigia simu na kunieleza kuwa basi alilotaka kusafiri nalo la Abood limejaa, basi alilopata ni Kimbinyiko. Basi nikamwambia akate hilohilo ili awahi chuoni.
“Kama dakika 15 zikapita nikasikia simu imeita kidogo ikakata, alikuwa Happiness, lakini nilipompigia hakupatikana. Baada ya saa mbili kupita nilimpigia mke wangu simu na kumweleza kuwa simpati mtoto kwenye simu, alinijibu kwamba bado hajarudi nyumbani,” alidai Francis.
Aliendelea kudai kuwa aliporudi nyumbani saa moja usiku, mke wake alimweleza kuwa Happiness alikuwa hajarejea nyumbani, lakini wakajipa matumaini kwamba huenda alikuwa amekwenda kwa marafiki zake. Wakala na kapumzika.
“Ilipofika saa sita usiku, mke wangu akaniamsha kuwa mtoto hajarudi, nilishtuka sana! Nikamwambia nenda tena kaangalie chumbani kwake, lakini binti yangu hakuwapo. Tukaanza kumpigia simu, ikaita tu pasipo kupokewa.
“Wakati tunaendelea kutafuta jinsi ya kufanya, ujumbe mfupi uliingia katika simu ya mke wangu kutoka kwa Happiness kuwa yupo kwenye wakati mgumu sana, alisisitiza ‘niombeeni na niagieni kwa wadogo zangu’, lakini hatukujua kama ujumbe huo ulitumwa na mtoto wetu au mtu mwingine,” alidai.
Alidai kuwa ujumbe huo, ulimshtua ndipo alipowapigia simu ndugu wa karibu wakafika nyumbani kwake kisha wakaenda Kituo cha Polisi Tandika, wakaturudisha tena kituo kidogo cha Sigara ambako walielezwa kuwa kuna mwili wa binti uliokotwa.
“Tulikwenda Kituo cha Polisi Chang’ombe tukaambiwa twende Hospitali ya (Rufani) Temeke kuhakiki mwili uliookotwa saa 12 alfajiri. Kwa kuwa muda wa mochwari ulikuwa umeshapita, wakatuambia twende siku iliyokuwa inafuata kwa ajili ya utambuzi. Siku hiyo niliweza kumtambua mwanangu.
“Tulirudi tena kituoni hapo kwa ajili ya kupata kibali cha kuchukua mwili, tukaambiwa mwili unatakiwa kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi. Tulipofika, tulielezwa kuwa mtoto aliuawa kwa kunyongwa shingoni. Basi tukachukua mwili, tukazika,” alidai
0 Comments:
Post a Comment