Monday 19 June 2023

Ntibazonkiza Katajwa Tena Hukooo

KIUNGO Fundi wa mpira anayetajwa kuviziwa na Simba, Hassan Nassoro ‘Machezo’ amemtaja kiungo nyota wa Msimbazi aliyeshinda tuzo za Mfungaji Bora, Kiungo Bora na Mchezaji Muungwana (Fair Play)’, Saido Ntibazonkiza katika kikosi bora cha msimu wa Ligi Kuu Bara uliomaliza karibuni.

Saido ametajwa kwenye kikosi cha Machezo ikiwa ni siku chache tangu nyota huyo kutoka Burundi aliyewahi kukipiga Yanga, kutajwa katika kikosi cha msimu kilichotangazwa kwenye Tuzo za TFF zilizofanyika Tanga, sambamba na mastaa wengine wa Simba, Yanga na Azam FC.

Machezo anayekipiga Mbeya City na aliyeshindwa kumaliza msimu kutokana na kulimwa kadi nyekundu kwenye pambano dhidi ya Yanga lililochezwa jijini Mbeya na kumalizika kwa sare ya 3-3 alikitaja kikosi chake bora kwa msimu huu, huku eneo la ushambuliaji alimtaja Saido aliyemaliza msimu akihusika na mabao 29, akifunga 17 na kuasisti 12.

Kiungo huyo anayemudu kucheza namba 6, 8 na 10 aliyewahi kukipiga Dodoma Jiji na timu ya taifa U23 alikipanga kikosi hicho akianza na kipa Diarra Djigui (Yanga) huku beki ya kulia akimpa Kenneth Kunambi (Mbeya City) na kushoto akimtaja Yassin Mustapha (Singida Big Stars).

Eneo la beki wa kati amempanga Ibrahim Bacca (Yanga) naAbdulrazak Hamza (Mbeya City), kwenye kiungo akijipanga yeye (Machezo), Salum Abubakar ‘Sure Boys’ (Yanga) na Bruno Gomes (Singida BS), huku winga ya kulia akimpa Richardson Ng’odya (Mbeya City) na kushoto Saido.

Machezo alimtaja mshambuliaji wake wa msimu ni Tariq Kiakala (Mbeya City) na upande wa kocha akimtaja Abdallah Mubiru anayemnoa Mbeya City inayojiandaa na mechi ya play-off ya kuepuka kushuka daraja dhidi ya Mashujaa mechi inayopigwa leo kabla ya kurudiana tena Juni 24.

Kuhusu mchezo huo, Machezo alisema anaamini ni nafasi ya kuiokoa Mbeya City isishuke daraja baada ya kukwama kujihakikisha kubaki Ligi Kuu mbele ya KMC iliyowafunga kwa jumla ya mabao 3-2.

“Malengo yangu ya kwanza ni kuisaidia Mbeya City kubaki katika ligi haukuwa msimu mzuri sana kwetu lakini naamini tutabakia, kisha ndipo dili zangu za usajili zifuate” alisema Machezo aliyekiri klabu kadhaa zimekuwa zikiwania saini yake ikiwamo Singida na Simba

0 Comments:

Post a Comment