YANGA wamemaliza msimu ikiwa ni timu iliyofanikiwa kuliko nyingine zote za Ligi Kuu Bara msimu huu.
Hii ni timu yenye mafanikio makubwa zaidi kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Kipindi hicho Yanga wamefanikiwa kutwaa makombe sita, lakini jambo kubwa zaidi ni kuhakikisha kuwa wamefika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, mafanikio ambayo ni makubwa.
Yanga walifikia mafanikio hayo baada ya kufanya usajili mzuri, kuwa na benchi zuri la ufundi ambalo limeweza kutumia nguvu kubwa kuhakikisha timu hiyo inakuwa na mafanikio hayo.
Hata hivyo, baada ya kumalizika kwa msimu huu Yanga wameanza kupitia sehemu ngumu kutokana na kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi kutangaza kuachana na timu hiyo kwa kuwa anahitaji chagamoto nyingine.
Nabi mwenye leseni kubwa ya UEFA Pro amefanya kazi nzuri baada ya kufanikiwa kuiongoza Yanga kwenye michezo 14 ya Kombe la Shirikisho Afrika, ameshinda michezo tisa, ametoka sare mitatu na kupoteza mitatu akiwa amekusanya jumla ya pointi 30.
Haya siyo mafanikio ya kwanza kwa Nabi kwani alishapita timu nyingine kubwa na kupata mafanikio makubwa na hivyo ameondoka akiwa anafahamu anakwenda wapi na kwanini.
Baada ya Nabi kutangaza kuondoka baadhi ya makocha wake wasaidizi wametajwa kuwa nao wanaondoka, jambo ambalo limeendelea kuzua maswali mengi kwa mashabiki wa soka.
Hata hivyo, Yanga wanatakiwa kuwa watulivu kipindi hiki kwa kuwa kuna baadhi ya wachezaji ambao nao wanaonekana wataondoka kwenye timu hiyo, huku wengine wakiwa hawana mikataba na wengine wanataka kupata changamoto mpya, hivyo watatakiwa kupambana kuhakikisha wanafanya usajili mwingine bora kwa ajili ya msimu ujao.
Jambo pekee ambalo linaonekana ni kwamba Yanga watalazimika kutumia fedha nyingi kama wanataka mafanikio kama ya msimu uliopita.
Wanaotajwa kuondoka ni Bernand Morrison ambaye mkataba wake na Yanga umemalizika, Tuisila Kisinda ambaye anacheza Yanga kwa mkopo na sasa anatakiwa kurudi kwenye timu yake Berkane ya nchini Morocco.
Mwingine ni Fiston Mayele, ambaye anatajwa kuwa anaweza kuuzwa na timu hiyo kutokana na timu kadhaa kubwa za Afrika kuweka fedha nyingi kwa ajili ya kumpata mfungaji huyo bora kwenye Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho Afrika.
Mbali na hawa pia Yanick Bangala, Djuma Shaaban, Joyce Lomarisa ni kati ya wachezaji ambao wana mkataba na timu hiyo, lakini wamepeleka maombi ya kutaka kuondoka.
Kipa Djigui Diarra, naye inatajwa kuwa anaweza kuondoka kutoka na kutakiwa na timu kadhaa kubwa Afrika, lakini bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Yanga.
Mbali na hawa, Yanga wanataka kuachana na Dickson Ambudo ambaye hajaonyesha kiwango bora msimu huu akitajwa kuwa anaweza kwenda Dodoma Jiji, kipa Erick Johora ambaye mkataba wake unamalizika, Denis Nkane ambaye atapelekwa kwa mkopo sawa na Abdalah Shaibu Ninja, David Bryson na Mamadou Doumbia ambaye ameshindwa kupata nafasi kwenye timu hiyo.
Wakati Yanga wanaonekana kuwa wana wachezaji kadhaa wakubwa wanaotakiwa kuondoka kwenye timu hiyo, bado inaonekana kuwa itabaki kwenye mhimili mzuri kwa ajili ya msimu ujao kama itafanikiwa kuzoa majina makubwa ambayo inatarajia kuyasajili.
Kauli ya Rais wa Yanga, Hersi Said baada ya kumalizika kwa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, alisema anaamini kuwa msimu ujao watakuwa na timu imara zaidi na watafanya usajili mkubwa ambao unaweza kuwapa mafanikio zaidi ya haya ya msimu huu.
Hata hivyo, baada ya majina makubwa yamekuwa yakitajwa kuwa yanaweza kwenda kufunika magepu ambayo yataachwa na wachezaji wanaoweza kuondoka kwenye timu hiyo.
Huyu ni mshambuliaji wa timu ya Al Hilal ya Sudan ambaye amekuwa kwenye ubora wa hali ya juu kwenye michezo kadhaa ambayo amecheza.
Lilepo ambaye alionyesha uwezo mkubwa wakati Yanga walipovaana na Al Hilal kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliomalizika. amekuwa akitajwa kuwa anaweza kujiunga na Yanga kwenye dirisha hili kwa mkopo.
Huyu ni kati ya wachezaji wachache wa ukanda huu ambao wanalipwa kiwango kikubwa cha mshahara na usajili wake ni ghali, hivyo Yanga wanamtaka kwa mkopo wa msimu mmoja na inaonekana watampata kutokana na changamoto ambayo ipo nchini Sudan kwa sasa ambayo imechangia ligi kusimama.
Tayari mazungumzo yameshaanza kati yake na Yanga, kama akifanikiwa kutua basi anaweza kuziba pengo la Mayele endapo ataondoka kwenye dirisha hili la usajili, mbali na kucheza nafasi ya mshambuliaji pia anaweza kucheza kushoto na kulia.
Huyu ni beki wa pembeni ambaye anaitumikia timu ya Asec Mimosas ambayo iliishia kwenye hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.
Vyanzo vinaonyesha kuwa mchezaji huyo anaweza kuziba pengo na mchezaji mmoja kati ya Joyce au Djuma Shaaban kama mmoja wao atafanikiwa kuondoka kwenye timu hiyo.
Huyu ni mmoja kati ya wachezaji mahiri wa Asec ambaye alitumika kwenye michezo mingi ya nyumbani kwenye michuano ya kimataifa msimu huu.
Mwaka 2018, thamani yake ilipanda kwenye soko hadi kufikia dola laki nne, lakini kwa sasa anapatikana kwa dola laki mbili ambazo ni sawa na shilingi bilioni 1.4, anaonekana kuwa beki mwenye uwezo mzuri lakini kwa mafanikio ambayo Yanga wanayataka hizi siyo fedha nyingi.
Huyu ni beki wa kushoto ambaye amekuwa akiwindwa na Yanga kwa kipindi kirefu akiwa anaitumikia timu ya KCCA ya Uganda, lakini ameshacheza nchi mbalimbali ikiwemo Ligi Kuu ya Canada, akiwa ameitumikia Montreal Impact.
Amekuwa bora kwenye michezo mingi aliyocheza, huyu ni kati ya mabeki wa pembeni wenye uwezo mzuri wa kupiga krosi na kutoa pasi za mabao.
Anaweza kuziba nafasi za Djuma Shaaban kama akiondoka kwenye timu hiyo, lakini pia ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa kwenye soka la Afrika.
Kwenye eneo la ulinzi wa kati Yanga hapaonekani kuwa na shida, lakini Yanga wanatajwa kutaka kumsajili beki huyo wa Mbeya City ambaye ni kati ya wachezaji waliocheza dakika nyingi zaidi msimu huu na msimu uliopita kwenye Ligi Kuu Bara.
Shemvuni ameonyesha kiwango kizuri kwa michezo yote muhimu ya Mbeya City msimu huu na msimu uliopita na inaelezwa kuwa Yanga wanataka kumsajili, ni kati ya wachezaji ambao walipomaliza mechi dhidi ya Yanga kocha Nasreddine Nabi alichukua namba yake.
Endapo Yanga watampata, anaweza kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo, lakini anaweza kupata kwenye michezo kadhaa ya FA na mingine ya Ligi Kuu Bara.
Vyuma hivyo vipya vitakutana na benchi jipya la timu hiyo kutokana na kuondoka kwa Nasreddine Nabi ambaye ameshatangazwa kuachana na klabu hiyo kama ilivyo kwa Kocha wa Makipa Mbrazili, Milton Nienov, huku kocha msaidizi, Cedric Kaze akiwa kwenye hatahati kutokana na kumaliza mkataba.
Tayari Yanga imekuwa ikihusishwa na makocha kadhaa wa kuja kuziba nafasi ya hao watakaondoka Jangwani akiwamo Florent Ibenge na Omar Najhi, huku Pitso Mosimane wa Afrika Kusini aliyekuwa akitajwa akiwa ameshalamba dili nono Falme za Kiarabu.
Makocha wote hao kila mmoja ana wasifu nzuri, lakini itategemea na mabosi wa Yanga na tajiri wao, GSM watakavyoamua kwa ni makocha wanaotajwa kuwa na gharama kubwa, hasa Ibenge baada ya Mosimane kutua klabu nyingine juzi.
0 Comments:
Post a Comment