MCHEZAJI Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Fiston Mayele, ameondoka rasmi kuelekea nchini Misri kwa ajili ya kukamilisha taratibu za mwisho na kusaini mkataba wa kuitumikia Pyramid FC.
Mayele ambaye alisaliwa na mkataba wa mwaka mmoja ndani ya Yanga, anatajwa kumalizana na matajiri hao wa Misri, Pyramid FC kwa ada ya usajili inayokadiriwa kuwa zaidi ya shilingi bilioni 2 za Kitanzania.
Chanzo chetu kutoka ndani ya Yanga ambacho kiko karibu na Mayele, kimeliambia Spoti Xtra kuwa, straika huyo ameondoka na kuelekea nchini Misri kwa ajili ya kumaliza taratibu za usajili na kusaini mkataba.
“Ni kweli Mayele leo (jana Jumatano) aliku2a akimalizia kufuatilia utaratibu za pasi yake ya kusafiria kwenye ubalozi wa Misri hapa Tanzania kwa ajili kuondoka nchini kwenda kukamilisha masuala yake ya usajili na kusaini mkataba.
“Kila kitu kuhusu dau la usajili na makubaliano binafsi kati ya mchezaji na timu zote mbili kimekamilika na huenda akatangazwa rasmi Ijumaa kuwa mchezaji rasmi wa Pyramid FC ya Misri,” alisema mtu huyo.
Mayele ni kati ya wachezaji ambao Yanga haikuwatambulisha katika Kilele cha Wiki ya Mwananchi sambamba na Djuma Shaban, Yannick Bangala na Mamadou Doumbia.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, hivi karibuni alisema: “Kuhusiana na Mayele na wachezaji wote ambao hawakutambulishwa kuwa sehemu ya kikosi kwa msimu mpya wa 2023/24 uongozi unatarajia kutoa taarifa rasmi hivi karibuni.”
Mayele ambaye ameitumikia Yanga kwa misimu miwili, amefanikiwa kuipa timu hiyo taji la Ligi Kuu Bara na Ngao ya Jamii mara mbili mfululizo msimu wa 2021/22 na 2022/23.
Msimu wa 2022/23, aliibuka kinara wa mabao katika Ligi Kuu Bara akifunga 17 sawa na Saidi Ntibazonkiza wa Simba. Pia alikuwa Mfungaji Bora wa Kombe la Shirikisho Afrika akifunga mabao saba wakati Yanga ikimaliza nafasi ya pili baada ya kupoteza mchezo wa fainali.
Kuondoka kwa Mayele, imeelezwa kwamba, Yanga inamsaka mbadala wake ikiangukia kwa Emmanuel Mahop raia wa Cameroon.
0 Comments:
Post a Comment