Saturday, 29 July 2023

Je Simba Wamejifunza?

Kikosi cha Simba Msimu wa 2022/23
Takwimu za msimamo wa Ligi Kuu ya NBC msimu uliopita zinaonesha licha ya kutokuwa mabingwa, Simba Sc imeongoza kwa takwimu za maeneo mengi dhidi ya mabingwa wa ligi hiyo, Yanga.

 

Takwimu zinaonesha Simba Sc ndiyo timu iliyofunga mabao mengi zaidi na kufungwa mabao machache zaidi, ikifunga mabao 75 na kufungwa mabao 17 huku ikifuatiwa na Yanga ambayo imefunga mabao 68 na kufungwa mabao 18, lakini pia Simba ndiyo timu iliyopoteza michezo michache zaidi, ikiwa imepoteza mchezo mmoja huku ikifuatiwa na Yanga iliyopoteza michezo miwili.

 

Unaweza kujiuliza, haya yote yamewezekanaje na timu hii ikakosa kuwa bingwa? Inafikirisha, kila mmoja ametoa dhana yake kulingana na mjadala huu huku wengi wakisema tatizo kubwa la Simba Sc ni kutokuwa na kikosi kipana jambo ambalo lilisababisha baadhi ya michezo iliyostahili kushinda kutoweza kushinda na kutoa sare zisizo na lazima hasa pale Mwalimu Roberto Oliveira Robertinho anapokuwa hana uwanda mpana wa kuchagua kikosi na kupumzisha baadhi ya majina, kuepusha athari za majeraha na uchovu. Je unajua kuhusu kikosi kipana?

 

KIKOSI KIPANA KIPOJE?

Kikosi kipana ni timu ambayo viwango vya wachezaji wake vinashabihiana au vinakaribiana kuanzia kwenye utimamu wa mwili, uwezo wa kiufundi wa mchezaji mmoja mmoja na uelewa wa mbinu za timu kiasi kwamba atakachokiwasilisha mchezaji anayepata nafasi mara kwa mara hakitofautiani kwa kiasi kikubwa na kile atakachokiwasilisha mchezaji asiyepata nafasi mara kwa mara.

 

Kuwa na kikosi cha kwanza kunachangiwa pia na kushabihiana kwa kocha mkuu na wasaidizi wake, nikimaamisha kuwa kocha wa viungo awawezeshe wachezaji kuwa timamu kimwili kuendana na mbinu za kocha mkuu, makocha wasaidizi wengine kama kocha wa makipa, kocha wa ufundi wa washambuliaji na wazuiaji waweze kuwafundisha wachezaji kuendana na mbinu za kocha mkuu na kadhalika.

 

JE, SIMBA HAIKUWA NA KIKOSI KIPANA?

 

Kwa sababu tumeshapata maana halisi ya kikosi kipana tunapata kung’amua kuwa Simba haikuwa na kikosi kipana kwa sababu ya utofauti wa viwango vya wachezaji wengi ambao walikuwa wakianza mara kwa mara na wale ambao hawakuwa wakianza mara kwa mara.

 

Baada ya kuwasili, Kocha Robertinho kwa asilimia zaidi ya 70 ya mechi za Simba kikosi cha wachezaji waliokuwa wakianza kilifanana na kilikuwa na uwasilishaji bora wa kimbinu uwanjani hii ikimaanisha kuwa waliendana na kocha huyu.

 

Simba kutokuwa na upana wa kikosi kulianza kuonekana pale tu kocha alipofanya mabadiliko ya kikosi cha wachezaji wanaoanza tofauti na wale ambao hawakuwa wakianza mara kwa mara, uwasilishaji wao uwanjani ulionekana kuwa na utofauti mkubwa kuanzia kiwango cha utimamu wa mwili, uwezo wa kiufundi na hata uelewa wa kimbinu wa kocha huyo.

 

Hii ikasababisha baadhi ya mechi ambazo Simba ilistahili kupata ushindi kutoa sare, mfano mchezo wa Simba dhidi ya Namungo. Kusema hivi siyo kupuuzia uwezo wa Namungo lakini kutoa uhalisia wa upana wa kikosi cha Simba kwani kwenye mchezo huo wachezaji walioanza wengi walikuwa ni wale ambao hawakuwa wakianza mara kwa mara.

 

Kikosi cha Simba kinachoanza mara kwa mara ni hiki; kipa Aishi Manula, mabeki wa pembeni ni Shomari Kapombe (kulia), Mohamed Hussein Zimbwe (kushoto), mabeki wa kati Henock Inonga na Joash Onyango, viungo wa kati Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin, viungo washambuliaji watatu nyuma ya mshambuliaji, Saidi Ntibanzokiza (kushoto), Kibu Denis (kulia) na Clatous Chama (kati) huku mbele yao wakiwa na mshambuliaji mmoja Jean Baleke.

 

Staili ya uchezaji ya Robertinho ni kuzuia kwa shinikizo kubwa kuanzia kwenye theluthi ya kuanzisha mpira ya wapinzani (High Pressing) na kushambulia kwa mashambulizi ya moja kwa moja (direct style of attack) huku akitumia mifumo tofauti wakishambulia na kuzuia, kama 4-1-4-1 kuzuia kuanzia mbele, 4-4-2 kuzuia kwenye theluthi yao ya pili na ya kwanza huku wakishambulia kwa muundo mama wa 4-2-3-1.

Haya yote huhitaji wachezaji timamu kimwili, wenye uwezo mkubwa kiufundi na uelewa mkubwa wa mbinu.

 

JE, SIMBA WAMETIBU TATIZO HILI?

 

Baada ya msimu kutamatika, Simba walifanya maboresho ya timu (Recruitment) kwa kuondoa majina ya wachezaji wengi ambao walikuwa hawatoi ushindani bora kwenye uwanja wa mazoezi dhidi ya wale bora kama Victor Akpan, Nelson Okwa, Augustine Okrah, Gadiel Michael, Erasto Nyoni, Jonas Mkude na Ismael Sawadogo.

 

Pia ikaondoa majina mengi ya wataalamu kwenye benchi la ufundi kama kocha wa viungo, Kelvin Mandla, kocha wa makipa, Zakaria Chlouaha na mtaalam wa misuli, Fareed Cassim ikiwa ni sambamba na kuajiri mkuu wa idara ya uskauti, Mels Dealers ambaye kazi yake kubwa ni kusimamia maingizo mapya kufidia nafasi zilizoachwa wazi.

 

Baada ya hapo, yakasajiliwa majina mengine mengi na bora kulingana na wasifu wa walikotoka huku imani yangu kubwa ikiwa ni kuwa watakuwa wamefanya kwa kuzingatia weledi kwani wana mkuu wa idara hiyo kwasasa ambaye anatimiza majukumu yake kulingana na mahitaji ya kocha mkuu.

 

Hivyo, baada ya hayo ni vyema sasa tusubiri uwasilishaji wa maingizo mapya kwani wengi wao tumewaona kwenye mechi chache ambazo timu zao zilikuja kwenye mashindano ya kimataifa au wengine kuwaona kupitia picha za video tu.

I

0 Comments:

Post a Comment