Tuesday 4 July 2023

NHIF Yakemea Matumizi Holela Ya Dawa

Mtwara. Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Bima ya Afya nchini (NHIF) Bernad Konga ameonya udanganyifu unaofanywa katika vituo vya afya huku akikemea matumizi holela ya dawa ambayo yanaweza kuleta madhara kiafya.

Kauli hiyo ameitoa leo katika mkutano wa wadau wa NHIF uliohudhuriwa Mwenyekiti wa bodi ya NHIF Juma Muhimbi ambapo alisema kuwa kumekuwa na matumizi holela ya dawa ambazo wagonjwa wanatumia bila kuonana na daktari.

Alisema kuwa unaweza kukuta mtu anaishi Mtwara anaagiza dawa Dar es Salaam kwa daktari wake na anatumia bila kuonana nae jambo ambalo linaweza kuwa ni hatari zaidi katika afya zao na hasa kwenye figo.

“Inawezekanaje utumie dawa ulizoletewa bila daktari kukupima na kujua kama zinakufaa ama la! Hii inaweza kuwa inachangia uwepo wa magonjwa ya figo nchini, unawezaje kutumiwa dawa tu na ukatumia utaratibu huu ambao siyo mzuri. Kawaida lazima mgonjwa aonane na daktarai kwanza ndio aandikiwe dawa gani anaweza kutumia,” amehoji na kuongeza;

“Yaani watu zaidi ya asilimia 15 tunatamani wapate huduma kupitia mfuko huu muwaelimishe ili tuwapate hamasa ya kulipia na kupata matibabu kupitia NHIF ambapo tunayomikakati ya kuwafikia watu ili kila mtanzania aweze kufikiwa na mfuko huu”

Meneja wa NHIF Mkoa wa Mtwara Dr Adolf Kahamba ambapo alisema kuwa udanganyifu huo umekuwa ukivigharimu vituo hivyo.

“Yapo makosa ambayo yanafanywa kwa kukusudia ambapo tukikuta makosa ya kukusudia tunayaondoa, udanganyifu unatuathiri pia; wanachelewesha malipo. Huwa tunafanya kaguzi kwa lengo la kuboresha huduma na kuwakumbusha watoa huduma na waajiri kutofanya udanganyifu,” amesema.

“Endapo tukihisi uwepo wa udanganyifu tunafanya ukaguzi wa kushtukikiza ambapo tukiukuta tunachukua hatua wale wanaofanya udanganyifu wa makusudi hatuachani nao hatua za kisheria zinaendelea”

“Udanganyifu sio mzuri sio kwenye vituo tu kuna mtu alifunga ndoa na dadake apate bima ya afya huu ni mmonyoko mkubwa wa maadili ndani ya jamii tukemee udanganyifu”

kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi NHIF Juma Muhimbi alisema kuwa Mfuko huo umejipanga kutoa huduma bora za afya na kuwasihi watanzania kujitokeza kujiunga kwa wingi zaidi.

“Sisi tunatoa huduma ya afya kwa wateja wetu mara kadhaa kumekuwa na changamoto, na njia pekee ya kupata taarifa za wanaopatiwa huduma na mfuko ni kukutana na kuzungumza ili kama kuna hitilafu ni nafasi nzuri ya kutusaidia kwenye uboreshai wa huduma zetu” alisema Muhimbi.

0 Comments:

Post a Comment