Wednesday 5 July 2023

Mwalimu Mkuu Kizimbani Kwa Kumbaka, Kumpa Ujauzito Mwanafunzi

Misungwi. Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Kilimo Wilaya ya Misungwi, Charles Maige (32) amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka ya kumbaka na kumpa ujauzito mwanafunzi mwenye umri wa miaka 15.

Akisoa hati ya mashtaka leo Julai 5, 2023 mbele Hakimu mkazi mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Misungwi, Amani Shao, mwendesha mashitaka wa polisi, Ramsoney Salehe amedai mshtakiwa alitenda kosa hilo siku isiyofahamika kati ya Machi na Aprili, 2023.

Mwendesha amedai mshtakiwa alitenda makosa hayo kinyume cha Sheria ya Makosa ya Jinai kifungu cha 130 (1) 2(e) na kifungu 131 sura 16 ya marejeo ya mwaka 2002.

Amedai ili kutimiza lengo lake, mshtakiwa alitumia kisu kumtishia mwanafunzi huyo kwa kutishia kumchinja shingo iwapo angepiga kelele wakati akimbaka.

Katika kesi hiyo ya jinai namba namba 92 ya mwaka 2023, mshtakiwa pia anadaiwa kumpa ujauzito mwanafunzi huyo kinyume cha Sheria ya Elimu kifungu cha 60 (A) (4) sura ya 353 ya marejeo ya mwaka 2002.

Akisoma maelezo ya kosa, mwendesha mashataka alidai ili kutimiza lengo lake, mshtakiwa alikuwa akienda nyumbani kwao mwanafunzi huyo na kujofanya kumtuma dukani kumnunulia gundi huku akimwagiza kumpelekea nyumbani kwake.

‘’Alipopelekewa gundi nyumnani kwake, mshtakiwa alimvutia ndani mwanafunzi wake na kumbaka huku akimtishia kwa kumwonyeshea kisu kilichokuwa mezani kwa kumwambia angemchinja akipiga kelele. Mshtakiwa alitumia njia hiyo kumbaka mwanafunzi wake zaidi ya mara tatu,’’ Mwendesha mashtaka ameieleza Mahakama

Mshtakiwa amekana mashtaka dhidi yake na shauri hilo limeahirishwa hadi Juali 10, 2023 ambapo mshtakiwa atasomewa maelezo ya awali baada ya upande wa mashtaka kuiambia Mahakama kuwa upelelezi umekamilika.

Hakimu Shao amemwachia kwa dhamana mshtakiwa baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya Sh10 milioni kila mmoja

0 Comments:

Post a Comment