Friday 28 July 2023

Usajili Mpya Wampa Jeuri Kocha Wa Yanga

HUKO ndani ya Yanga, unaambiwa mambo yameanza kuiva, hiyo ni kutokana na Kocha Miguel Angel Gamondi kutamba na timu yake hiyo haswa katika eneo la kiungo ambapo kuna mafundi wa maana.

Yanga wamefanya usajili wa wachezaji wawili wenye uwezo mkubwa wa kucheza namba 10 ambao ni Maxi Mpia Nzengeli na Zouzoua Pacome kupitia dirisha hili kubwa.

Akizungumza na Spoti Xtra, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, alikichambua kikosi cha timu hiyo na kusema kuwa, Kocha Gamondi kutokana na ubora wa wachezaji alionao katika eneo la kiungo, basi atasumbua sana msimu ujao kutokana na uwezo wa wachezaji hao kuwa mkubwa.

“Nataka niwaibie siri kubwa sana haswa katika eneo la kiungo la Yanga, ukiangalia usajili wa msimu huu utabaini kuwa kuna ongezeko la wachezaji wawili ambao wanaweza kucheza kama namba 10 jambo ambalo msimu uliopita halikuwepo.

“Msimu uliopita kulikuwa na Azizi Ki pekee yake katika eneo la namba 10 au kiungo mshambuliji, lakini kwa ujio wa Pacome na Maxi ni wazi kuwa msimu ujao Yanga chini ya Kocha Gamondi watu wataseka sana kwa kuwa faida kubwa ya hawa wachezaji ipo haswa katika kufunga mabao na kutengeneza mabao pia,” alisema kiongozi huyo.

0 Comments:

Post a Comment