Friday 7 July 2023

Wafumaniwa Wakifanya Ngono Kanisani, Ibada Zasitishwa

Uganda. Kundi la waumini wa Kanisa la Bungonya lililoko wilayani Kayunga nchini Uganda wamesusia shughuli za ibada baada ya watu wawili kufumwa wakifanya mapenzi ndani ya kanisani hilo.

Jumanne Julai 5,2023, Saa 2 usiku, mwanaume huyo (23), anayedaiwa kuwa mwanandoa na baba wa watoto wawili alifumwa na mwanamke ambaye alitalakiwa na mumewe siku chache zilizopita na kulazimika kuishi kwa bibi yake katika kijiji hicho.

Tukio hilo la kushtusha, liliibuliwa na mke wa ndoa wa mwanaume huyo ambaye baada ya kumkuta mumewe akifanya mapenzi ndani ya kanisa alipiga kelele (Yowe) iliyowafanya waumini kujaa na kuwakamata watu hao wakiwa utupu.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la nchini Uganda, tukio hilo limewafanya viongozi wa kanisa hilo kuingia katika mfungo na maombi yasiyokuwa na ukomo ili kukemea kitendo hicho walichokitaja kama “Dhambi ya kushtusha”.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Bungonya lilipotokea tukio hilo, George William Kanda alisema watu hao waliingia kanisani kupitia dirishani kabla ya kuanza kufanya tukio hilo.

“Waliingia kanisani kupitia dirishani kwa sababu mlango ulikuwa umefungwa,” alisema

“Mke wa ndoa wa mwanaume huyo alipowafumania alipiga kelele watu wakajaa kanisani na kuwakamata watu hao kisha kuwaleta ofisini kwangu. Mtandio wa kichwani na fulana (t-shirt) ya mwanaume vimehifadhiwa kwa Mwenyekiti kama udhibitisho,” alisema Kanda

Kanda aliongeza kuwa baada kufikishwa walihojiwa kisha kuachiwa, huku kesi hiyo ikitarajiwa kuendelea kusikilizwa

Ofisa Uchunguzi wa Makosa ya Jinai katika wilaya ya Kayunga nchini humo, Beatrice Ajwang pamoja na kukiri kusikia kisa hicho alisema hakuna kesi iliyowasilishwa ofisini kwake.

Kiongozi wa Kanisa la Bugonya Uganda, Aaron Komugisha alisema kanisa limeandaa hafla itakayokutanisha viongozi wa kanisa wilayani humo kuliombea kanisa na kuliweka wakfu kabla ya shughuli za ibada kurejea.

“Viongozi waliotembelea kanisa hili walishtushwa na kitendo hicho,” alisema Aaron

“Watu hao wanatakiwa kutubu dhambi zao mbele ya Mungu,” alinukuliwa mmoja wa shuhuda wa tukio hilo.

Kijiji cha Bugonya kipo takribani Kilometa 35 kutoka mjini Kayunga.

0 Comments:

Post a Comment