Dodoma. Serikali imesema inafanya mapitio kwa ajili ya kuhuishwa sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015.
Hayo yamesemwa leo Juni 20, 2023 na Naibu Waziri wa Habari, Mawasaliano na Teknolojia ya Habari, Methew Kundo wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Neema Lugangira.
Mbunge huyo alihoji Serikali ina mpango gani wa kuhuisha Sheria ya Makosa ya Mtandao na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi pamoja na mkataba wa Malabo.
Akijibu swali hilo, amesema Serikali imekamilisha utungwaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022 iliyosainiwa Novemba, 2022 na kutangazwa katika gazeti la Serikali Desemba 2 Desemba, 2022.
Amesema Sheria hiyo imeanza kutumika Mei, 2023.
Amesema Serikali imeweka mazingira wezeshi zaidi ya utekelezaji wa masuala mbalimbali yanayohusiana na Tehama ikiwemo kufanikisha kufikia azma ya uchumi wa kidijitali.
Amefafanua mazingira hayo ni Serikali kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP) inaendelea na zoezi la mapitio ya Sera, sheria, na mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa inayohusu Tehama,” amesema.
“Sheria zinazofanyiwa mapitio kwa ajili ya kuhuishwa ni pamoja na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015. Vile vile mikataba ambayo utaratibu umeanza kwa ajili ya kuridhiwa ni pamoja na Mkataba wa Malabo,” amesema.
0 Comments:
Post a Comment